Na Mwandishi Wetu, Pwani
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Jenista Mhagama, ameridhishwa na maendeleo ya mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa kwa lengo la kukuza ujuzi katika fani mbalimbali kwa vijana Mkoa wa Pwani.
Jenista ametoa kauli hiyo leo, alipotembelea na kukagua shughuli za utekelezaji wa programu hiyo katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Wilaya ya Kibaha.
Waziri ameridhishwa mafanikio kwa wanafunzi waliojiunga katika fani mbalimbali, ufundi wa kushona, useremala,kutengeneza majokofu na viyoyozi, ufundi umeme wa majumbani na umeme wa magari.
“Nimefurahishwa na kundi la vijana kujitokeza kuongeza ujuzi bila kujali viwango vya elimu zao, kwani katika awamu hii, wapo walioshindwa kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na wahitimu wa elimu ya juu wanaoendelea na mafunzo ya ufundi stadi hapa VETA”, amesema.
Aidha amezipongeza jitihada za uongozi wa chuo kwa kushirikiana na ofisi yake kuendesha mafunzo hayo kwa kuamini yatasaidia kuendeleza jitihada za kutatua changamoto za ajira nchini.
“Nimekuja kutizama maendeleo ya mafunzo haya na kuona changamoto zinazowakabili ili kuzitatua kwa namna bora na kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki ya kujifunza kulingana na umuhimu wa mafunzo na kuyafikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Jenista.
Akiwasilisha taarifa ya chuo hicho pamoja na utekelezaji wa programu hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA ,Clara Kibodya, ameeleza mafanikio ya uwepo wa mafunzo ambapo, vijana wameweza kupata ujuzi, walimu kupata fursa ya kuzitumia fani zao, ongezeko kubwa la vijana wa kike hasa katika fani zilizoaminika na jamii kuwa za kiume pamoja na mafunzo kusaidia kupunguza wimbi la vijina wasio na ajira.