25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI: FARU JOHN ALIKUFA

johnie

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa juzi saa  7:00 usiku alipokea inayoeleza kuwa faru maarufu kwa jina la John alikufa tangu Agosti 18, mwaka huu.

Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya Majaliwa kutaka kupewa maelezo iwapo faru huyo yuko hai au alikwishakufa.

Akitoa taarifa hiyo juzi usiku nyumbani kwa Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema afya ya faru John ilianza kuzorota tangu Julai 10, mwaka huu.

Alisema faru John alihamishwa kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti, Serengeti, mkoani Mara ili kuruhusu kuongezeka kwa faru weusi.

Profesa Maghembe alieleza kuwa hadi Desemba 2015 wakati faru huyo anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa faru John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Profesa Maghembe.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa na Profesa Maghembe mbele ya Waziri Mkuu iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.

Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.

“Nilipokea taarifa yenu jana (juzi) saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo (jana) tukimaliza sherehe za Maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,” alisema Majaliwa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alikabidhi pembe za faru huyo kwa Waziri Mkuu.

Mande alisema kuwa pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa NCAA kuwa hadi kufikia Desemba 8, uwe umempelekea nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru huyo na kama amekufa apelekewe hata pembe zake.

Waziri Mkuu aliituhumu menejimenti, wafanyakazi wa NCAA na baraza la wafanyakazi NPC kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi.

Alisema asingeweza kuvumilia sakata la faru huyo aliyedai kuwa alikuwa na taarifa kuwa alihamishwa kwa siri kwenda V.I.P Grumet Desemba 17, mwaka jana ambako waliahidiwa kupatiwa Sh. milioni 200 na tayari walikuwa wamepatiwa Sh.  milioni 100 kama fedha za awali.

Hata hivyo baadhi ya tarifa ambazo zilikwisharipotiwa kwenye gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) zinaeleza kuwa tayari maofisa watano wa NCAA wanaotuhumiwa kushiriki kumhamisha faru John walikamatwa kwa mahojiano ili kujua ukweli wa mazingira ya kuondolewa kwake.

Taarifa zinadai kuwa faru huyo mweusi alizaliwa mwaka 1978 na wazazi wanaoitwa Betty na Hamisi.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles