21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ASAMEHE WAFUNGWA 5,678

wafungwa

NA HARRIETH MANDARI

RAIS Dk. John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 5,678, ambapo 1,340 wataachiwa  huru, huku 4,338 wakinufaika kwa kupunguziwa kifungo na kubaki gerezani wakitumikia  sehemu iliyobaki.

Rais Dk. Magufuli alitoa msamaha huo jana, katika maadhimisho ya Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara,  kwa kutumia madaraka aliyopewa na  katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 45(1) (d).

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kutoa msamaha huo baada ya mwaka jana kufuta sherehe za uhuru.

Mwaka 2014, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alitoa msamaha kwa wafungwa 4,129 na mwaka 2013 alitoa kwa 3,814.

Wafungwa waliofaidika na msamaha wa sasa ni baada ya kupunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kusainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira, ni mategemeo ya Serikali kuwa watakaochiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Aidha, katika msamaha huo, wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao, zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu namba 49(1) cha sheria ya Magereza Sura ya 58, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i-xx).

Wafungwa waliopata msamaha ni wale wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na saratani, ambao wako kwenye hatua ya mwisho na ambao wamethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya.

Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya, wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu wao umethibitishwa na jopo la waganga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, msamaha huo hautawahusu  wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani, pia wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Wengine ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya, makosa ya uombaji, upokeaji na utoaji rushwa, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo.

Wengine ni wanaotumikia kifungo cha makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo, waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea.

“Makosa mengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo, wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act no. 25/1994) na sheria ya Huduma kwa jamii (Act no. 6/2002),” ilieleza taarifa hiyo.

Vilevile wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, waliopunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na  bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Pia wafungwa waliopatikana na hatia ya makosa ya utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu na pia wafungwa waliopatikana na hatia ya kukutwa na viungo vya binadamu.

Makosa mengine ambayo hayahusiki na msamaha huo ni ya wafungwa waliojihusisha na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha za Serikali, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali na pia wafungwa walioingia gerezani baada ya Oktoba 9, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles