27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Waziri Biteko awashukia waliompora ardhi mjane

Na Mwandishi Wetu-Geita



NAIBU Waziri wa Madini, Doto Biteko amewashukia viongozi wa Kijiji cha Ngula wilayani Geita kwa kumnyang’anya mjane ardhi yake yenye madini licha ya kukaa eneo hilo tangu mwaka 1954.

Baada ya viongozi hao kumnyang’anya mjane huyo ardhi yake, walianza kupokea gawio kutoka kwa Kampuni ya Nyati Resources inayofanya shughuli za uchimbaji dhahabu katika kijiji hicho.

Biteko aliitaka kampuni hiyo kusitisha mara moja kutoa gawio la umiliki wa ardhi kwa Serikali ya Kijiji hicho kama ilivyokuwa ikifanya.

Akiwa katika ziara yake kwenye mgodi huo wa Ngula kukagua shughuli za uchimbaji madini, kusikiliza na kutatua kero zinazohusu sekta ya madini, Biteko alikutana na mjane Mindi Masasi (80), ambaye alimweleza namna alivyodhulumiwa ardhi yake yenye madini.

Masasi alisema yeye ndiye mmliki halali wa ardhi hiyo na aliishi hapo na mumewe ambaye sasa ni marehemu tangu mwaka 1954, lakini baada ya madini kubainika, uongozi wa kijiji ulidai ardhi hiyo ni yake na ikaanza kupokea mapato katika eneo hilo.

Alisema mwaka jana Kampuni ya Nyati Resources ilipoanza kuchimba madini kwenye eneo hilo ilikuwa ikimlipa gawio la umiliki wa ardhi, lakini Aprili mwaka huu Serikali ya Kijiji cha Ngula ilidai kumiliki ardhi hiyo na hivyo kuanza kupokea gawio kutoka kwa kampuni hiyo.

Kutokana na malalamiko hayo, Biteko alimwagiza Meneja wa Kampuni ya Nyati Resources, Christopher Nilla, kusitisha utoaji wa gawio hilo hadi pale tume huru ya uchunguzi itakapoundwa na kutoa majibu sahihi nani mmiliki wa ardhi hiyo inayokadiriwa kufikia heka 350.

“Mnasema hii ardhi ni ya kijiji, kwanini hamkuchukua huko kwenye mihogo mkaona hapa tu kwenye madini ndiyo kwenu, haiwezekani mfanye uonevu kwa mama huyu kwa sababu tu mnyonge.

“Mnachukua maamuzi yenu kisha mnasambaza habari kila mahali mkijua huyu bibi hawezi kufika huko, hili haliwezekani,” alisema Biteko.

Biteko alisema fedha hizo zinazopelekwa kwenye Serikali ya kijiji, kuna madai kuwa zinatumiwa vibaya hivyo akataka suala hilo lichunguzwe.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngula, Symphorian Michael, alisema alichukua uamuzi wa kuweka zuio kwa Kampuni ya Nyati Resources kutoa gawio kwa Masasi baada ya vikao vyote vya kutafuta mmiliki halali wa ardhi hiyo kukaa na kubaini kwamba eneo hilo ni la Serikali ya Kijiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles