NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amezindua mradi wa umeme wa kilowati 430, unaotokana na maporomoko ya maji katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe.
Kutokana na mradi huo, mpaka sasa zaidi ya wateja 1140 wameunganishiwa umeme.
Alisema mradi huo umetekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya CEFA kutoka Italia na kugharamiwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na Serikali ya Tanzania kwa Dola za Marekani 110,209.
Alisema mradi huo utasambazwa katika vijiji vilivyoko kata za Ikondo, Matembwe na Lupembe na ziada itakayobaki inaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
” Habari njema, tayari vijiji Saba vimeunganishiwa umeme kupitia mradi huu, malengo ya Serikali ya kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati bora katika maeneo ya vijijini kupitia asasi za kiraia,” alisema Dkt. Kalemani.
Alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, dadi ya wananchi wanaopata huduma ya umeme imefikia asilimia 40, huku vijijini ikiwa ni asilimia 24 na kueleza  kuwa juhudi zaidi zinafanyika ili kufikia lengo la kuunganisha umeme kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025.
Naye Meneja Mradi wa CEFA, Jacopo Pendezza, alisema taasisi hiyo ipo nchini kutoka mwaka 1976 imejikita katika miradi ya umeme vijijini.
Alisema umeme wa Ikondo ulikuwa unazalisha kilowati 80 za umeme, lakini kutokana na mahitaji ya wananchi kuongezeka, CEFA kwa kushirikiana na Kampuni ya Kijiji cha Matembwe (MVP) inayosimamia mradi huo, waliamua kuongeza mtambo wa kilowati 350 na kufanikiwa kuzalisha kilowati 430.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa EU, Jenny Nunes, alisema mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi, kusaidia wanafunzi katika masomo na huduma nyingine muhimu za kijamii na kusaidia juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi, alisema  makao makuu ya wilaya zote mkoani Njombe yameunganishwa na huduma ya umeme huku vijiji 250 kati ya 384 vinapata huduma hiyo.