23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI ANAWEZA KUTOA KIBALI MTOTO MGENI KUPATA URAIA


Na LEORAD MANG’OHA

SHERIA ya uhamiaji imeweka wazi kuwa mzazi au mlezi ambaye ni raia wa Tanzania mwenye mtoto asiye raia wa Tanzania anaweza kumwombea uraia kwa waziri mwenye dhamana.

Utaratibu wa kumwombea mtoto mgeni uraia wa Tanzania ni tofauti na utaratibu unaotumika kwa mgeni mtu mzima na hivyo hauhitaji kupitia katika ngazi ya kata, wilaya au mkoa.

Mwanamke yeyote wa kigeni mtu mzima mwenye akili timamu aliyeolewa na raia wa Tanzania anaweza kuomba uraia wa Tanzania kwa waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia.  Masharti na utaratibu wa kuomba uraia wa Tanzania kwa wanawake walioolewa ni mwombaji lazima awasilishe ombi lake wakati wa uhai wa mumewe pamoja na ushahidi wa uwapo wa uhusiano wa kindoa na uthibitisho wa uraia wa mume wake.

Pia mwombaji lazima awasilishe ushahidi wa uhalali wake wa kuwa Tanzania na anatakiwa kujitangaza katika magazeti ya Kiswahili na Kiingereza yaliyosajiliwa Tanzania kuonesha nia yake ya kuomba uraia wa Tanzania ili jamii iweze kupata fursa ya kutoa maoni kuhusu mhusika.

Utaratibu wa kuwasilisha maombi kwa wanawake wa kigeni walioolewa na raia wa Tanzania hauhitaji kupitia katika taratibu za ngazi ya kata, wilaya na mkoa ili kuweza kuwasilisha ombi hilo kwa waziri.

Ombi la uraia kwa mwanamke mgeni aliyeolewa na raia wa Tanzania linapokuwa limekamilika hupelekwa moja kwa moja kwa waziri mwenye dhamana likiwa na mapendekezo kwa ajili ya uamuzi.

Kama ilivyo kwa raia wengine wa kigeni, pia anatakiwa kuukana uraia wa nchi yake au wa nchi nyingine alionao na kutoa tamko la maandishi na kuapa kiapo cha utii. Hii ni kwa sababu Tanzania hairuhusu uraia wa nchi mbili au zaidi.

Pia anapaswa kufanyiwa uchunguzi kwa kuchukuliwa alama za vidole, ili kuona kama aliwahi kufanya makosa yoyote ya jinai.

Uraia wa nchi mbili ni dhana inayomruhusu mtu kuwa na uraia wa mataifa mawili au zaidi.  Dhana hii kwa Tanzania imekuwapo tu kwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18 na kwamba anapofikisha umri wa miaka 18 anapaswa kuukana uraia wa nchi nyingine aliokuwa nao ili kuweza kuendelea kutambulika kama raia wa Tanzania.

Aidha, anapaswa kutoa kiapo cha utii na kusajili tamko lake kuhusiana na nia yake ya kuishi Tanzania.  Zipo namna mbili ambazo dhana ya uraia wa nchi mbili inaweza kuhisiwa kuwapo Tanzania ambazo ni mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania akiwa na mzazi mmoja ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au tajnisi, pili ni mtu ambaye amezaliwa ndani ya Tanzania akiwa na mzazi mmoja ambaye ni raia wa nchi nyingine.

Dhana hii ni hisia tu, iwapo mtu huyo ataweza kuthibitisha kuwa pamoja na kuzaliwa nje ya Tanzania hana uraia wa nchi nyingine, hitaji la kuukana uraia huo halitakuwa la msingi kwake.

Kwa upande mwingine dhana hii iwapo itathibitika kuwa mtu huyo ana uraia wa nchi nyingine na ameshafikisha umri wa miaka 18 atapaswa kuukana uraia wa nchi hiyo nyingine na kutoa kiapo cha utii ili aweze kuendelea kuwa raia wa Tanzania na pasipo kufanya hivyo atakuwa ameukana kuwa raia wa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, atahitaji kuwa na kibali halali cha uhamiaji kitakachomwezesha  kuishi nchini kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ana uwezo baada ya kupata kibali cha waziri kuongeza muda wa kuukana uraia wa nchi nyingine kwa mtu yeyote ambaye ataonesha sababu zinazoridhisha kuhusu kuchelewa kuukana uraia wa nchi nyingine.

Muda huo unaongezwa kwa nia ya kumpa nafasi mtu huyo kufanya kile ambacho hakuwa amekifanya ili kuweza kutambulika kama raia wa Tanzania.

Ikumbukwe kuwa mtu yeyote aliyezaliwa nje ya Tanzania na mzazi (baba au mama) ambaye wakati anazaliwa mtu huyo mzazi wake alikuwa nje ya nchi kwa shughuli za kibalozi, mtu huyo anahesabika kuwa ni Mtanzania na hivyo hatahitajika kuukana uraia wa nchi yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles