29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Waziri akabidhiwa majina ya watumishi hewa 2,000

PICHA NO.2Veronica Romwald na Asifiwe George, Dar es Salaam

WAKUU wa Mikoa wamewasilisha ripoti ya awali ya watumishi hewa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ikionyesha ni zaidi ya  2,173.

Mkoa wa Mwanza unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa   334 huku katika Mkoa wa Shinyanga ripoti hiyo ya awali ikionyesha  hakuna   watumishi hewa.

Wakiwasilisha taarifa zao kwa waziri, wakuu hao wa mikoa kwa nyakati tofauti, walisema katika idadi hiyo walibaini wengine walikuwa tayari wamehamishwa lakini walikuwa wanaendelea kulipwa katika vituo vyao vya kazi.

Baadhi ya watumishi ingawa wamekwisha kufariki dunia,   bado majina yao yamo kwenye orodha ya malipo na serikali imekuwa ikiwalipa huku wengine wakiwa ni watoro, walisema.

Katika ripoti hiyo, Mkoa wa Arusha umetajwa kuwa na watumishi hewa 270 walioisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.188, Dodoma 101 (Sh  milioni 287.316), Dar es Salaam 73 (Sh.milioni 316), Iringa 15, Kagera 14 ambao walilipwa Sh milioni 49.147, Katavi 21 (Sh milioni 20.79), Kigoma 171 (Sh milioni 114.68), Kilimanjaro 111 (Sh milioni 281.475).

Mkoa wa Lindi   watumishi hewa saba na watoro 57 waliosababishia serikali hasara ya Sh milioni 36.213, Manyara 55, Mara 94, Mbeya na Songwe 98, Morogoro 122, Mtwara 17, Ruvuma 37, Pwani 150, Rukwa 18, Simiyu 62, Singida 202, Tabora 48 na Tanga 104.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti kutoka kwa wakuu wa mikoa 26, Waziri Simbachawene alisema   idadi hiyo itajumuishwa pamoja na fedha ambazo zimetumika kuwalipa na ripoti kamili itawasilishwa  kwa Rais Dk. John Magufuli.

“Tumieni mamlaka yenu kuwafikisha katika vyombo vya dola watu hawa walioisababishia serikali hasara, nitashangaa kama mtakuja kuomba msaada kwetu wa kuwashughulikia.

“Wananchi wanataka kujua hawa mliowataja wanachukuliwa hatua zinazostahili,” alisema.

Simbachawene aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanazisimamia halmashauri zao vizuri kwa kudhibiti mrundikano wa watumishi wa umma katika maeneo ya mijini.

“Nimefanya uhakiki nikabaini kuwa kuna idadi kubwa ya watumishi wa umma mijini kuliko vijijini nikashangaa kwa nini hasa walimu… nendeni mkafanye ukaguzi na kulishughulikia suala hili.

“Kuna uzalishaji mwingi wa madeni huko kwenye halmashauri, kwa mfano, mwalimu anaidai serikali fedha za likizo, matibabu au uhamisho wakati ameitumikia halmashauri kwa muda mrefu na kulingana na mapato ya halmashauri husika wana uwezo wa kumlipa lakini wanamuwekea deni ili serikali kuu imlipe, jambo hili haiwezekani,” alisema.

Aliagiza wakuu hao  kusimamia kwa mkakati suala la uanzishaji wa viwanda vidogo ili kuzalisha ajira kwa vijana na kuhakikisha kila mkoa unaweza kufikia kiwango cha uchumi wa kati.

“Kuna maeneo mengi yana matatizo lakini kuweni wabunifu… tunatarajia ushindani kwenu katika kutatua changamoto zilizoko kwenye mikoa yenu, hasa katika sekta ya afya na elimu.

“Nakiri kwamba katika bajeti iliyopita halmashauri hazikupata fedha katika mtiririko mzuri uliopangwa hali iliyoleta changamoto kubwa na kusababisha baadhi ya miradi  mingi ya maendeleo kusimama kutokana na mchakato wa Katiba Mpya ambao ulichukua fedha nyingi na Uchaguzi Mkuu .

“Lakini   serikali hii ya awamu ya tano imedhamiria kwamba lazima fedha hizo zifike kwa wakati, simamieni vizuri maana itawekeza fedha nyingi kwenye miradi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles