22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa, wasomi waijadili MCC

Peter-MsigwaNA FLORIAN MASINDE,DAR ES SALAAM

SIKU mbili baada ya Bodi ya Shirika la ufadhili la Changamoto za Millennia (MCC), kutangaza kufuta msaada wa Dola za Marekani milioni 472 (zaidi ya Sh trilioni moja) kwa Serikali ya Tanzania, wasomi na wadau wa uchumi wametoa maoni tofauti kuhusiana na suala hilo.

Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, alitangaza kuunga mkono hatua ya Bodi hiyo akisema  nchi yake itaendelea kusaidia serikali katika maeneo mengine hususan sekta za afya na elimu licha ya bodi kufuta msaada huo ambao ulikuwa unagusa moja kwa moja miundombinu ya nishati ya umeme vijijini.

Kutokana na hatua hiyo, wadau wamesema kuna kila dalili ya kuathirika kwa bajeti ijayo ya serikali kwa kuwa fedha hizo huwa zinalenga katika ujenzi wa barabara za vijijini na kusambaza umeme sehemu hizo.

Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Mataifa, Mchungaji Peter Msigwa, alisema upinzani umesikitishwa na Tanzania kukosa fedha za MCC ambazo zilitarajiwa kuharakisha upatikanaji wa umeme vijijini.

Taarifa ya Mchungaji huyo ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema, ilikosoa kauli iliyotolewa na Serikali kwamba haijatishika na hatua hiyo ya Marekani.

Alisema  MCC inazingatia vigezo katika kuchagua nchi inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo hivyo ni nchi kuwa na dhamira ya dhati kuimarisha demokrasia na kuendesha uchaguzi   huru na haki.

“Serikali ilifahamu vizuri vigezo vinavyostahili lakini inashangaza kuona Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni wanadiplomasia mzoefu akilitia aibu Taifa kwa kulalamika kuwa kaonewa.

“Kauli ya Waziri ya kukata makosa yaliyo dhahiri yaliyofanywa na serikali ya CCM inaweza kuweka rehani uhusiano na ushirikiano mzuri wa demokrasia ambao Tanzania imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa kama MCC,” ilisema taarifa hiyo ya Msigwa.

Wasomi nao wanena

Mhadhiri Mwandamizi wa Shule kuu ya Elimu Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Joviter Katabaro, alisema kuna athari kubwa kwa taifa.

Alisema kufutwa kwa msaada kunaweza kusababisha mataifa na taasisi nyingine zinazofuatilia na zimekuwa zikitoa misaada kwa Tanzania,   kuanza kuwa na shaka na serikali iliyopo.

Dk. Katabaro alisema: “Unapotegemea msaada hasa kwa mataifa makubwa kama Marekani unakuwa kwa namna moja umeuza uhuru wako kwa sababu ili uweze kupata msaada huo lazima ufuate masharti na matakwa yao hata kama yanakukandamiza.

“Barabara, umeme na maji siyo peke yake vinavyoathirika na hatua hiyo ya Bodi ya MCC bali hata sekta nyingine kama elimu, afya, kilimo na biashara zitaathirika kwa kuwa zote zinategemeana”.

Msomi huyo alisema  Tanzania si mara ya kwanza kufungiwa misaada huku akitoa mfano wa miaka ya 1960 ambako Ujerumani ilisimamisha misaada yake kwa serikali lakini badaye ilirudi na kuendelea kutoa misaada yao. Hata hivyo, alisema ni jukumu la serikali kujipanga upya na kuendeleza miradi iliyokuwa inategemea msaada huo.

Mtaalamu wa uchumi ambaye pia ni Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema kuna athari kubwa katika uchumi zitakazotokana na hatua hiyo ya MCC kwa kuwa fedha hizo zilikuwa zinalenga kuinua uchumi hasa   vijijini.

Profesa Ngowi alisema: “Kama taifa tusiogope kujifunza tunapokuwa tegemezi na tuwe tayari kubeba gharama zetu wenyewe   inapotokea hali kama hii.  Hivyo tujipange na kupambana katika kukusanya mapato na kutumia vyanzo vyetu vya ndani kujiendesha”.

MCC ilifuta msaada na kuiondoa Tanzania katika orodha ya nchi zinazotakiwa kupata misaada hiyo baada Zanzibar kufuta uchaguzi wa Oktoba mwaka jana pamoja na Tanzania kutunga sheria ya makosa ya mitandao kugandamiza uhuru wa kujieleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles