26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aja juu daktari kupigwa

nani.Na Waandishi Wetu, Dar,  Mtwara

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kuhakikisha ndugu wa mgonjwa waliompiga daktari akiwa kazini, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za  sheria.

Ummy pia alikemea tabia ambayo imejengwa hivi karibuni nchini ya baadhi ya wananchi kuwapiga madaktari na wauguzi.

Aliyasema hayo jana katika ujumbe wake alioandika kwenye ukurasa wake wa ‘Twitter’.

Alieleza kusikitishwa na kitendo hicho alichofanyiwa Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula mkoani Mtwara, Dickson Saini.

“Ninakemea tabia hii inayotaka kujengeka dhidi ya madaktari… nimewasiliana na RC Mtwara (Halima Dendegu) na yeye ameshaagiza wahusika wakamatwe,” alisema.

Tukio hilo lilitokea juzi ambako ndugu wa mgonjwa mmoja ambaye alifikishwa hospitalini hapo baada ya kupata ajali ya pikipiki  walimpiga Dk. Saini.

Wananchi hao walimpiga daktari huyo baada ya kumwandikia mgonjwa huyo kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya.

Baada ya tukio hilo, wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo walitishia kutotoa huduma wakipinga mwenzao kupigwa.

Daktari huyo anadaiwa kupigwa na kuvuliwa nguo na ndugu hao ambao walikuwa wakilazimisha ndugu yao asiandikiwe rufaa ya kwenda Muhimbili badala yake  aandikiwe kwenda hospitali nyingine   Masasi au Lindi.

Mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini, walisema   ndugu wa mgonjwa walimpiga daktari huyo baada ya kuwapa taarifa ya vipimo vya mgonjwa wao kuhitajika kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuwa alikuwa amevunjika taya.

Walisema  ndugu hao wa mgonjwa walidai  warudishiwe gharama za matibabu walizotoa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo siku moja kabla ya kupewa rufaa.

“Hali ya mgonjwa haikuwa nzuri alihitaji matibabu ya hali ya juu ambayo kwa hapa hayapo ndiyo maana daktari aliyekuwa akimuhudumia aliona ni vema kutoa rufaa   akapate matibabu yanayostahili,” walisema mashuhuda hao.

Akizungumzia tukio hilo, Dk. Sahini alisema siku ya tukio alitembelea wodi aliyolazwa mgonjwa huyo na kumwandikia vipimo kikiwamo cha X-ray huku akiendelea na matibabu ya nyama kabla ya kuanza yale ya mifupa.

“Kwa kawaida matibabu ya mfupa ni lazima kutibu kwanza nyama kabla ya mfupa na katika X ray tuligundua mgonjwa huyo alivunjika taya, niliwaita ndugu zake na kuwaeleza amevunjika taya na matibabu yake ni Muhimbili.

“Nilikwenda kumuona mgonjwa kama kawaida na alishaandikiwa vipimo (x-ray) na alianza kupatiwa matibabu ya nyama kabla ya mfupa.

“Baada ya kuona vipimo, niliwaleza nitawaandikia waende Muhimbili wakaanza kulalamika kwa nini isiwe Nyangao au Ndanda, nikawaambia sifahamu matibabu yao siwezi kumtoa mgonjwa hospitali ya rufaa nimpeleke ya chini,” alisema daktari huyo.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Shahibu Maarifa alipoulizwa kuhusu kusimamishwa  huduma hospitalini hapo, alisema  alikuwa mbali na akaomba apewe muda afuatilie suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles