Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema kusipokuwa na umakini wa mifuko ya plastiki katika kipindi cha miaka ijayo, bahari itajaa mifuko hiyo kuliko samaki.
Hayo yalielezwa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akifungua mkutano na wadau wanaozalisha mifuko ya plastiki nchini.
Wadau hao watatoa maoni yao yatakayo kuwa na lengo la kudhibiti uharibifu wa mazingira ambayo yatafanyiwa uchambuzi kisha wizara kutoa uamuzi sahihi kwa manufaa ya nchi.
Alisema mifuko hiyo imejaa katika mito na bahari huku wataalamu wakitoa maoni yao kuwa kutakuwa na mafuriko ya mifuko hiyo baharini kuliko samaki na viumbe hai wengine.
“Kutokana na jambo hili tumeamua kukutana na wadau wanaozalisha mifuko ya plastiki hapa nchini ambao watatoa maoni yao yatakayo kuwa na lengo la kudhibiti uharibifu wa mazingira ambayo yatafanyiwa uchambuzi kisha wizara kutoa maamuzi sahihi kwa manufaa ya nchi na si vinginevyo,’’ alisema Makamba.
Alisema mifuko hiyo haiozi lakini husagika na kubaki chembechembe ndogo ambazo zinaingia kwenye chakula cha samaki.
“Hivyo pia upo uwezekano kwa siku za usoni watu kula minofu ya samaki yenye chembechembe za plastiki hizo jambo ambalo ni hatari kwa afya za binadamu,” alisema.
Aliongeza kuwa kadri siku zinavyoendelea kutakuwa na matatizo ya watu kushindwa kutofautisha unene wa mfuko wa plastiki unaotakiwa kuzalishwa hapa nchini lakini pia tatizo litaendelea katika kuziba kwa mifereji .
“Ni imani yangu kuwa maoni yatakayotolewa yatakusanywa vizuri na kupelekwa wizarani na kufanyiwa uchambuzi kisha kufanya maamuzi yaliyosahii kwa manufaa ya nchi na kutolewa maamuzi muafaka yatakayoleta tija kwa taifa,’’ alisema Makamba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kutengeneza mifuko ya plastiki cha Wande Printing&Packaging Company Limited, Joseph Wasonga, alisema wapo tayari kushirikiana na Serikali katika suala la kudhibiti uingizwaji wa plastiki iliyochini ya kiwango.
Kwa ujumla hakuna mifuko ya plastic iliyosalama kwa afya ya binadamu.Dawa ni mmoja tu ni kipiga marufuku uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastics.