33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza kukamatwa kigogo Wizara ya Maji

Na Elizabeth Kilindi-Njombe

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani hapa kumkamata kigogo wa wizara hiyo, Goyagoya Mbena kwa tuhuma za kughushi nyaraka kwa kushirikiana na wahandisi wa maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Wasimamizi hao na wakandarasi wa miradi ya maji ya Ukarawa na Ihang’ana wanadaiwa kutumia fedha za miradi hiyo sambamba na kutekelezwa chini ya kiwango.

Aweso pia ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Loishiye Ngotee ambaye kwa sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Agizo hilo alilitoa jana mkoani hapa wakati wa kikao cha tathmini ya baada ya ziara katika miradi hiyo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Alisema kuna baadhi ya vigogo wamekuwa wakighushi nyaraka kwa niaba ya katibu mkuu na kwamba ni lazima wakamatwe wafikishwe katika vyombo vya dola.

“Nimegundua kwamba kuna baadhi ya watu wizarani wanahusika kughushi nyaraka kwa niaba ya katibu mkuu ilihali si katibu mkuu, na sisi kama viongozi wa wizara hatuna haja ya kuwaonea haya.

“Tumekwisha chukua hatua, kuna baadhi tumeshawafukuza kazi, lakini hawa wengine waliohusika niwaombe wakuu wa mikoa na wilaya yoyote mnayehisi anahusika katika wizara hii, sisi tunatoa ushirikiano katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa dhidi yao,’’ alisema Aweso.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka aliwaomba wenyeviti wa halmashauri kuwa makini katika usimamizi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

“Niwaombe wenyeviti wa halmashauri na kamati zao za kukagua miradi mjiridhishe kabla ya kutokea matatizo ambayo yanasababisha kupoteza fedha nyingi za Serikali,’’ alisema Sendeka.

Miradi ya maji katika vijiji vya Ukarawa na Ihang’ana imekamilika zaidi ya miaka sita iliyopita, lakini wakazi wa vijiji vinavyonufaika na miradi hiyo hawajawahi kupata huduma ya maji hadi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles