32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wazee Chadema wahofia chama kufutwa

Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee la Chadema, Roderick Lutembeka, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kumsihi  Rais Dk. John Magufuli, kuwasikiliza viongozi wa dini pamoja na viongozi wa chama hicho.Kulia ni mjumbe wa baraza hilo Naomi Kaihula, na mjumbe mwingine, Alfred Ntupewa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee la Chadema, Roderick Lutembeka, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kumsihi Rais Dk. John Magufuli, kuwasikiliza viongozi wa dini pamoja na viongozi wa chama hicho.Kulia ni mjumbe wa baraza hilo Naomi Kaihula, na mjumbe mwingine, Alfred Ntupewa.

NA MAULI MUYENJWA,DAR ES SALAAM,

BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema),limedai kuwa kuna njama za kutaka kukifuta chama chao.

Katibu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka, alidai kuwa kwa mujibu wa taarifa za uhakika walizozipata kutoka moja ya taasisi nyeti za Serikali, mpango huo ulipangwa kutekelezwa baada ya maandamano ya Ukuta Septemba Mosi, mwaka huu.

“Mtiririko wa matukio ya hivi karibuni kupitia Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa, kuna njama zilizolenga kukihujumu Chadema kwa kuandaa mitego haramu ya kisiasa ili hatimaye yatolewe mapendekezo ya kukifuta katika orodha ya vyama vya siasa.

“Msajili wa Vyama vya Siasa aliitisha kikao ambacho kingefanyika Agosti 29 na 30 kujadili mambo mbalimbali, likiwamo kuzuiwa kwa shughuli za vyama vya siasa kufanya mikutano ya nje na ndani.

“Siku mbili kabla ya kikao hicho kufanyika, ilitolewa kauli nyingine kupitia Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo kuwa kikao kilichopangwa kufanyika Agosti 29 na 30 kimeahirishwa hadi Agosti 3 na 4 mwaka huu,”alisema Lutembeka.

Katibu huyo alisema kuwa hawakupewa barua hata moja kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kuwaita katika kikao chochote kati ya hivyo vilivyotangazwa kufanyika na hata hicho kilichoahirishwa.

“Jambo hili ni kinyume cha taratibu za mawasiliano rasmi ya kiofisi baina yetu na Ofisi ya Msajili ambayo yote hufanyika kwa barua. Lakini inavyoonekana baada ya kutangaza kusitisha maandamano yetu ya Septemba 1, hakukuwa na haja ya kikao hicho ambacho kingesaidia kutatua changamoto za kidemokrasia zilizopo.

“Ni matumaini yetu kuwa njama hizi zitapingwa na watu wote wapenda amani kwa uamuzi huo unaoweza kusababisha machafuko ya kisiasa nchini na kuzalisha vikundi vya kutetea demokrasia kwa njia isiyo rasmi, jambo ambalo sisi kama nchi hatupaswi kuliacha litokee katika ardhi yetu,”alisema.

Baraza hilo pia ilitoa ushauri kwa Rais John Magufuli kuwa mwangalifu wa kauli anazozitoa kwa umma kwani zinaweza kuleta mpasuko wa kitaifa.

Akizungumza na MTANZANIA juu ya madai hayo ya wazee wa Chadema, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monika Laurent, alisema kama wana ushahidi wa kuwapo kwa njama hizo, wathibitishe hadharani.

Alisema kuwa Msajili wa Vyama vya siasa ni mratibu tu wa Baraza la Vyama vya Siasa hawezi kuingilia uamuzi wa kamati ya uongozi.

Alisema kuwa Mwenyekiti ambaye anachaguliwa na wajumbe wa baraza hilo ndiye anayekuwa na uamuzi katika uongozi wa baraza hilo.

“Msajili yeye hana nguvu yoyote ya kushawishi kamati ya uongozi isipokuwa mwenyekiti ambaye anachaguliwa na wajumbe wa baraza hilo ndiye anayekuwa na uamuzi katika uongozi wa baraza hilo,” alisema.

Alisema kuwa Msajili alipendekeza tarehe ya mkutano huo na dhumuni lake ilikuwa kujadili mwenendo wa demokrasia, si kuzungumzia Ukuta.

Alisema kuwa sababu za kuahirishwa kwa mkutano wa Agosti 29 na 30 ilikuwa ni suala lililo nje ya uwezo kwani muda ulikuwa hautoshi kuwaandaa wadau wote waliotakiwa kuhudhuria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles