29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAZAZI WATAKIWA KUPINGA UDHALILISHAJI WATOTO

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Najma Murtaza Giga, amewataka wazazi na walezi kuunga mkono juhudi za Serikali na wanaharakati katika kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa wazazi katika Mkoa wa Mjini, uliofanyika Amaan Unguja.

Alisema wazazi ndio walezi na waangalizi wa malezi ya makundi yote katika jamii, hivyo ni lazima wawe mstari wa mbele kupinga vitendo vyote vinavyoenda kinyume na maadili, mila desturi na utamaduni visiwani humo.

“Hii ni vita yetu sote, kila mzazi amuone mtoto wa mwenziwe kama wake, hapo ndipo tutakapoweza kuwalinda watoto wetu ili wakue katika malezi bora yasiyokuwa na vikwazo vya kukatisha malengo yao ya baadae.

“Wanawake na watoto wengi wamekuwa ni wahanga wa kubakwa, kulawitiwa na kutelekezwa hali inayosababisha wengi wao kuathirika kisaikolojia, ” alisema Najma.

Aliwasihi wazazi, viongozi wa dini na wanasiasa nchini kuhakikisha wanakemea kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya vijana wanaovaa nguo zinazokwenda kinyume na utamaduni sambamba na kutumia lugha zisizofaa katika jamii.

Akizungumzia uchaguzi wa mikoa mbalimbali, aliwataka wajumbe kuwachagua viongozi imara na wenye dhamira ya kweli katika kuleta mabadiliko na maendeleo ndani ya CCM na jumuiya hiyo.

Aliwasisitiza wasimamizi wa uchaguzi huo kutenda haki na wapigakura kuwa na uadilifu wakati wa kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wanaowataka bila ya kufanya vurugu.

Alisema jumuiya hiyo ina majukumu mawili makubwa ya kuhakikisha CCM inashinda na kubakia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 sambamba na kusimamia maendeleo ya elimu, malezi, utamaduni na mazingira kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles