23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wamlilia Jafo mimba shuleni

BENJAMIN MASESE-SENGEREMA

WANANCHI wa Kijiji cha Chifunfu wilayani Sengerema mkoani Mwanza wamemwomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo kwenda wilayani humo kushuhudia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chifunfu wanavyotembea kilomita 19 kwenda shuleni.

Walisema hali hiyo imesababisha wanafunzi wengi wa kike kupata mimba zisizotarajiwa.

Ombi hilo walilitoa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shule mpya ya Sekondari Bugumbisiko ambako pia walimtuhumu diwani wa kata hiyo, Robert Madaha (CCM) kuwa anakwamisha jitihada zao kutokana na itikadi za siasa.

Walisema licha ya kujitolea na kujenga shule nyingine ya sekondari Bugumbisiko, lakini haijaezekwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, hivyo kusababisha watoto wao kupata mimba na kukatisha masomo yao kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule.

Wakizungumza huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wananchi hao walidai kuwa diwani huyo amekuwa  akifanya fitina ndani ya vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kutoa kauli za kukwamisha ujenzi wa Sekondari ya Bugumbisiko.

Akisoma taarifa za Kamati ya Ujenzi wa Sekondari ya Bugumbisiko, Katibu wa kamati hiyo,  Fredick Nyamwanda alisema wananchi waliamua kuanzisha ujenzi wa shule hiyo baada ya shule ya kata iliyopo sasa kujengwa mbali na kijiji hicho ambapo watoto hutembea kilimito 19 ili kufika na wengi hushindwa kumaliza masomo kutokana na mimba zinazotokana na vishawishi na mazingira yasiyokuwa rafiki kwao.

Nyamwanda alisema kutokana na adha hiyo, wananchi wa vitongoji vitatu kati ya tisa,  waliamua kuanzisha ujenzi huo ambao vyumba sita vya madarasa vimekamilika huku nyumba ya mwalimu, maabara, jengo la utawala na ujenzi wa shimo la choo  ukiwa katika hatua za mwisho kukamilika.

“Hadi sasa ujenzi ulipofikia tumetumia Sh milioni 29.7, lakini kutokana na uongozi wa kijiji na kata kutokuwa karibu, kamati imepata wakati mgumu kupata pesa za kumalizia kutokana na kauli zinazotolewa na viongozi wetu, ujenzi umeingiliwa na imekatisha tamaa wananchi na wadau wengine kutochangia,” alisema.

Vicent Magembe ambaye ni mjumbe wa Serikali ya kijiji, alidai kuwa diwani huyo hana nia nzuri na shule hiyo, kwamba amekuwa akiweka vikwazo ngazi ya wilaya ili isiezekwe.

Diwani Madaha alikanusha kukwamisha ujenzi huo, huku akidai kuwa amekuwa akijitahidi kumshawishi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema ili kuezekea madarasa hayo ili shule iweze kusajiliwa na kuanza masomo mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles