27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aonya wanaoendesha makao ya watoto

Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya wamiliki na waendeshaji wa makao ya watoto ambao hawafuati taratibu za usajili wa watoto hao, kuwatumia kama mitaji au masilahi binafsi na wanaoendesha makao hayo kwa minajili ya kidini na kikabila.

Alisema hayo juzi Dar es Salaam, wakati wa futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima.

Aliwataka pia wamiliki hao waache kuwalea watoto hao katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya Kitanzania na maofisa ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja katika usajili wa watoto ili kuhakikisha wanaostahili ndio wasajiliwe kwenye makao hayo.

“Nitoe rai kwamba watu mmoja mmoja, taasisi na makao wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za uendeshaji wa makao kama vile mtoto kukuzwa katika mazingira ya familia, kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya misingi ya tamaduni za kigeni.

“Mtoto kukuzwa kwa kuzingatia masilahi bora ya mtoto, kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika dini ya mtoto na utamaduni wake, kutotenganisha watoto na ndugu na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki, kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji na kutunzwa na kuendelezwa hadi kufikia kimo cha utimilifu wao,” alisema.

Majaliwa alitumia hadhara hiyo kutoa maelekezo mahsusi kwa waendeshaji wa makao na wasimamizi wa sheria na taratibu za uendeshaji wa makao ya watoto yatima.

 “Taasisi na makao zihakikishe kuwa kila mtoto anawekewa mpango maalumu wa kuondoka kwenye makao na namna ya kumuunganisha mtoto huyo na familia yake.

 “Wamiliki wa taasisi na makao, waruhusuni maofisa ustawi wa jamii na maofisa wengine wa Serikali wafanye ukaguzi kwa mujibu wa sheria na wekeni utaratibu wa kuandaa taarifa za kila mwezi za watoto na taarifa ya mwaka wa fedha,” alisema.

Wengine walioonywa ni wale wanaowabadili watoto dini kinyume cha sheria, wanaofanya vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto, wasiowaruhusu watendaji wa Serikali kufanya ufuatiliaji na usimamizi, wasioandaa mpango wa kuwaunganisha watoto na familia zao na hivyo kusababisha watoto kukaa kwa muda mrefu kwenye makao na wale wanaondesha makao bila kuwa na leseni ya uendeshaji.

Majaliwa alisema Serikali haitowafumbia macho watu wa namna hiyo, na mara tu watakapogundulika kuanzisha au kuendesha makao bila kufuata taratibu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema tangu mwaka 2016 hadi sasa, kuna jumla ya watoto 24,067 wanaolelewa katika makao yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao 140 yanayoendeshwa na kumilikiwa na watu au taasisi binafsi. Kati yao wavulana ni 11,925 na wasichana ni 12,142.

Majaliwa alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu upatikanaji wa huduma za msingi kwenye makao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

 Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa bima ya afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

 “Hadi sasa watoto 900 kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha wamepatiwa kadi hizo na zoezi hilo linaendelea,” alisema.

Alisema Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu uendeshaji wa makao ya watoto sambamba na kutoa elimu kuhusu malezi, makuzi, haki, ulinzi na usalama wa mtoto kwa mujibu wa sheria zinazosimamia haki na ustawi wa mtoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles