26 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wahimizwa kuacha ukeketaji

Na Malima Lubasha, Serengeti                                       

AFISA Maendeleo ya Jamii wilayani Serengeti mkoani Mara, Sunday Wambura amewataka wazazi na walezi wilayani humo kuacha kuendekeza tabia za ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni na ukeketaji kwa watoto wa  shule za Msingi na sekondari kwani tabia hizo zinakatisha ndoto za watoto wengi.

OFISA MAENDELEO YA JAMII WILAYA YA SERENGETI , SUNDAY WAMBURA (KUSHOTO) AKIZUNGUMZA NA WAZAZI, WALEZI NA WANANCHI WA KIJIJI CHA KISANGURA AKIZUNGUMZA NAO ILI WAACHE KUWAFANYIA VITENDO VYA UKATILI WATOTO WA KIKE WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI HASA UKEKETAJI NA NDOA ZA UMRI MDOGO 

Wambura alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisangura wilayani hapa na kuelezea changamoto mbalimbali za ukatili wa kijinsia wanazopata watoto wa kike wanapokutana na vitendo hivyo pamoja na hatua zilizochukuliwa na wilaya kukabiliana na changamoto hiyo. 

Alisema ukeketaji umechangia kwa kiwango kikubwa kukatisha masomo kwa watoto wa kike kwani wengi wao huishia kuwaozesha kabla ya umri unaokubalika kisheria na wengine kuathirika kiafya kutokana na kutokwa na damu nyingi, kupata kovu la kudumu sehemu za siri, kuathirika kisaikolojia, na kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa kwa kuchangia vifaa vya ukeketaji.

Alisema, anatambua maandalizi ya ukeketaji kwa msimu huu yameshaanza tayari licha ya serikali na asasi za kiraia kuendelea kukemea vikali mila hiyo yenye athari kwao na kandamizi na kusisitiza kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na mamlaka zingine imejipanga kikamirifu kuzima mchezo huo mchafu.

“Nawahimiza wazazi wote wilayani hapa, acheni ukeketaji, badala yake hakikisheni mnapeleka watoto wa kike shule ili taifa liweze kupata wataalamu wa fani mbalimbali kwani kitendo mnachofanya kimepitwa na wakati na hakina maana yeyote kwa mabinti zetu.

“Naamini kupitia mkutano huu mmepata elimu na ufahamu mpana na kutambua madhara ya ukeketaji, hivyo niombe muwe mstari wa mbele kufichua na kuwasaidia wasichana ambao wapo katika hatari kubwa ya kukeketwa na muweke mikakati thabiti ya kuwanusuru na ukeketaji kabla hawajafanyiwa vitendo hivyo,” alisema Wambura.

Aidha, Wambura aliwahimiza walezi wote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na  usalama kuwalinda watoto kama ambavyo sheria ya mtoto inaelekeza ili elimu iliyotolewa iwe chachu ya kupunguza ndoa za utotoni na aina yeyote ya ukatili wa watoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles