VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM
WAZAZI wameshauriwa kulala na watoto wao hasa wanapotembelewa na wageni majumbani mwao, kama hatua ya kuwalinda dhidi ya ukatili wa kingono (ulawiti na ubakaji).
Rai hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa Kongamano la Kujadili Masuala ya Haki za Watoto katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya hakiya mtoto yaliyofanyika jijini hapa.
Waziri Ummy alisema ni vema wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao ili kuwalinda dhidi ya vitendo hivyo.
“Inasikitisha mno kwani vitendo hivi kila siku vinatokea kwenye jamii yetu, mambo yamebadilika, watoto wanalawitiwa na kubakwa na ndugu wa karibu majumbani,” alisema.
Alisema kila siku anapokea simu na ujumbe mfupi wa maandishi akijulishwa taarifa za watoto kubakwa na kulawitiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Lazima niseme ukweli, sijui tumekosea wapi, viongozi wa dini naomba mtusaidie kukemea hili kwenye jamii, watoto usiku wanageuzwa, inasikitisha.
“Tumeweka sheria miaka 30 jela lakini bado watu wanafanya, hivyo sheria si mwarobaini wa kumaliza hili, tutatumia sheria lakini lazima tuelimishe jamii.
“Takwimu za utafiti wa hali ya afya na watu na viashiria vya malaria (TDHS-MIS) 2015/16 zinaonesha wasichana balehe wanne kati ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 wamefanyiwa ukatili wa kingono kati ya umri wa miaka 15 hadi 19.
“Takwimu zinaonesha mtoto mmoja kati ya wawili wa kike na wa kiume wa umri kati ya miaka 13 hadi 19 wamefanyiwa ukatili wa kimwili.
“Mtoto wa kike mmoja kati ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kingono na mwalimu wake na asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 tayari wamezalishwa,” alisema.
Alisema takwimu zinaonesha pia wasichana watatu kati ya 10 wamabakwa au kulawitiwa na kwa upande wa watoto wa kiume ni mmoja kati ya saba.
“Si salama nyumbani, mtaani na hata shuleni, tunahitaji kuwalinda… Lakini hii kazi si ya serikali peke yake ni jukumu la kila mmoja lazima tufanye kazi kwa pamoja,” alisisitiza.
Alisema Serikali imekusudia kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama katika shule zote za umma na binafsi ili kudhibiti hali hiyo.
“Tunakusudia pia kuanzisha agenda ya kitaifa ya kusukuma mbele afya na ustawi wa wasichana lengo ikiwa kuwalinda dhidi ya ukatili, mimba na ndoa za utotoni, lishe duni na kupunguza kiwango cha maambukizi ya HIV ambacho kinaonesha kipo juu kwa wasichaana ikilinganishwa na wavulana,” alisema.
Aliwahimiza watoto kujifunza kwa bidii huku akiwasisitiza wasichana kwamba maendeleo ya mwanamke hayaji kwa uzuri wa sura wala umbo.
Awali akizungumza, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Watoto, (UNICEF), Maniza Zaman, alisema takwimu zinaonesha watoto ndilo kundi kubwa nchini hivi sasa.
“Ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania na inakadiriwa idadi hii itaongezeka ifikapo 2030 na bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukatili wa kimwili na kingono, lazima juhudi zifanyike kuwalinda,” alisema.
Mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Chang’ombe, Vanessa Innocent, aliiomba Serikali kuwapima watoto kwa uwezo waliojaaliwa (vipaji) badala ya matokeo ya darasani pekee.