25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wazaliwa wa Kata ya Ijumbi wajitolea kujenga Zahanati

Na Nyemo Malecela, Kagera

Wananchi waliozaliwa katika Kata ya Ijumbi wilayani Muleba mkoani Kagera ambao wanaishi mikoa mbalimbali na nje ya nchi wamejitolea kujenga zahanati ili kuwanusuru wenyeji wa kata hiyo waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.

Wananchi hao wakiongozwa na Prosper Rweyendera maarufu kama ‘Mzee PR’ wamekabidhiwa majengo matatu yatakayotumika kama zahanati hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ambaye aliambatana na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Wilaya hiyo, kata na Kijiji.

Baada ya Nguvila kupokea majengo hayo ameahidi kuanza ukarabati hivi karibuni kwa sababu tayari Sh milioni 30 zimetengwa na Wilaya hiyo kwa ajili ya kumalizia ukarabati huo.

Nguvila alisema ufadhili huo uliotolewa na Mzee PR ni sadaka kwa watoto wa Ijumbi na jamii kwa ujumla.

“Najiuliza, wilaya hii ya Muleba inao wasomi wengi, majaji, maprofesa madaktari, wahandisi wengi, wametawanyika ndani na nje ya Wilaya ya Muleba, Ulaya na Amerika wapo, Dar es Saalam, Arusha, Dodoma na wengine wana vyeo vikubwa, mbona hawakumbuki nyumbani?

Mimi naamini kama wangekuwa wanakumbuka nyumbani Wilaya ya Muleba tusingepata taabu, tungekuwa matajiri kweli kweli, kama ni wasomi, tarafa ya Nshamba ndio wamejaa, lakini tunamuona Mzee PR na wengine wachache ndio wanachapa kazi,” alisema Nguvila.

Aliongeza, “Mzee wangu, nasema hivi kwa namna unavyojitolea, Mungu akubariki sana, Mungu aendelee kukupa umri mrefu, mbali na kufanya haya, unayoyasaidia kwenye jamii kupitia sekta hii ya afya na maeneo mengine ambayo unachangia, siyo rahisi kwa mtu wa kawaida lakini mtu ambaye anajua nini maana ya uasili wake, unachokifanya hiki kiwe mfano kwa wengine,” amesema Nguvila.

Nguvila alisema inawezekana kuwa ngumu kwa wengine kukuelewa anachokifanya Mzee PR, lakini huduma wanayoenda kuipata wananchi kupitia zahanati hiyo wataelewa mawazo yake mema aliyonayo kwa jamii.

“Ni wangapi wakishatoka nje ya Tanzania wanakumbuka asili yao? Kuna mabilionea wenye asili ya Ijumbi wanaishi nje ya Tanzania lakini hata watoto wao hawaijui Ijumbi ilivyo,” amesema Nguvila.

Pia amempongeza Numerianus Marco Mulokozi ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Ijumbi wilayani humo kuwa kwa kitendo cha kukumbuka kurudi kuwekeza nyumbani ni cha kizalendo ukilinganisha na umri wake.

“Kwa umri wako bado unakumbuka kuja kusherekea sikukuu za Noeli na mwaka mpya ukiwa nyumbani kwenu kwa hakika Mungu akubariki sana.

Tungepata watu 10 Kama wewe Mbuge hasingepata kazi ngumu ya kutatua shida zote zinazolikabili jamii,” amesema.

Amesema kitendo cha kuwalipia ada na vifaa vya shule kwa wanafunzi tisa wenye kipato cha chini ni jambo jema, ambalo halitasaulika katika jamii.

“Umechangia ujenzi wa shule katika shule ya msingi Ijumbi, kompyuta na simtanki kwa shule ya sekondari Ijumbi na kutoa motisha kwa watakaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

“Pia endapo utapata fursa ya kupata vifaa tiba kama vitanda vya kujifungulia wakina mama na vinginevyo tunaomba umshirikishe mbunge na Mkuu wa Wilaya ili kuangalia uwezekano wa kupunguziwa kodi wakati wa kuviingiza nchini Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Mzee PR alisema majengo hayo yanatosheleza kuwa kituo cha afya lakini kutokana na maelekeza ya serikali imeshauriwa kusajiliwa kama zahanati.

Alisema wamefikia maamuzi ya kujenga zahanati hiyo ili kuondoa changamoto ya kupata huduma ya afya kwa jamii ambayo ndio chimbuko lao licha ya kuishi mikoa mingine kutokana na majukumu ya kikazi.

“Tunazijua changamoto za Ijumbi, tumeamua kuwekeza nyumbani ili baada ya kumaliza shughuli zetu kwenye miji tunayofanyia kazi na kuamua kurudi nyumbani sisi na wajukuu wetu tusione tufauti ya kimazingira tukilinganisha na tulipotoka.

Mbali na kujenga zahanati lakini pia tumeshiriki kujenga, kituo cha Polisi, mahakama na shule,” alisema Mzee PR.

Amesema yeye na wafadhili wengine wataendelea kushirikiana kutafuta fedha na ufadhili ili kuhakikisha wanaboresha mazingira ya Ijumbi na kuwa sawa na miji mikubwa.

Naye Marco ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Kata ya Ijumbi wilayani humo alisema maisha aliyoishi wakati akisoma katika shule ya msingi Rubya Mseto ndio yaliyopelekea kurudi nyumbani na kuwekeza katika elimu.

Alisema aliwahi kusoma katika darasa lililokuwa na wanafunzi 157 kitu ambacho kilimuuliza na kuamua kuwekeza katika elimu ili kupunguza changamoto hiyo kwa watoto wa ndugu zake wanaoishi kijijini huko.

Hadi sasa Marco ametoa shilingi milioni moja kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo, kompyuta, simtenki la maji, ada na vifaa vyote vya shule kwa wanafunzi tisa ambao walikabiliwa na changamoto ya kukosa ada.

Pia atawasomesha wanafunzi hao hadi wao watakapofikia kikomo cha kusoma wakati huo huo akiwa ametenga fungu la fedha kwa ajili ya kutoa motisha kwa wanafunzi wote watakaopata ufahulu wa daraja la kwanza na la pili katika mitihani ya taifa lengo likiwa kuongeza ufahulu.

“Wapo watanzania wengi wenye uraia wa Marekani wanaohitaji kusaidia walikotoka lakini wanakabiliwa na changamoto ya kupoteza uraia wa Tanzania,” alisema.

Diwani wa Kata Ijumbi, Wilbad Kakuru alisema msaada wa ujenzi wa zahanati hiyo utaweza kuhudumia wanakijiji 1,1000 wa kata ya Ijumbi na wengine kutoka Kata jirani za Ibuga, Buangaza, Buganguzi na Kashasha.

Alisema kwa sasa kata hizo zote hazina zahanati wala kituo cha afya hivyo zimekuwa zikitegemea kupata huduma kutoka kituo cha afya cha Rubya.

“Ili kukamilisha ukarabati wa zahanati hiyo tayari Halmashauri ya Muleba tayari imetenga shilingi milioni 30 katika bajeti ya mwaka 2021/2022,” amesema.

Wakati naye Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Nshamba, Devotha Katabarwa alisema msaada wa zahanati hiyo utapunguza changamoto ya vifo vya wakina mama wajawazito na kujifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wanaotembea kutoka vijiji vya milimani ambako miundombinu ya usafiri ni shida ata kama watapewa gari la kubebea wagonjwa.

“Uwepo wa zahanati hiyo utapunguza kiwango cha udumavu wa watoto kwani wanawake wengi wamekuwa wakishindwa kupeleka watoto wao kliniki kwa sababu ya umbali,” alisema.

Naye mwananchi Sara Resirwa ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Dodoma lakini ameishi mkoani Kagera kwa miaka sita alisema wamekuwa wakipata changamoto ya usafiri wakati wa usiku inapotokea watoto wameugua gafla.

“Awali tulikuwa na duka la dawa ambalo lilikuwa likitusaidia tunapopata dharura ya ugonjwa wakati wa usiku lakini kwa sasa limefungwa.

Hivyo endapo zahanati hiyo ikikamilika itatusaidia pale watoto wakiugua usiku kwani wataweza kupata huduma ya afya kwa urahisi, lakini itapunguza hatari kwa wanawake wanaojifungulia nyumbani kwa kutumia wakunga wa kawaida.”

Sara alisema imekuwa kawaida kwa wananchi wengi kujifingulia nyumbani kutokana na kukosa usafiri wa uhakika wa kwenda kwenye kituo cha Afya cha Rubya ambacho ndicho kipo karibu.

Naye Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo alisema tayari ameshawasiliana na Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu ili kumueleza jinsi walivyosaini mkataba wa makubaliano na wafadhili ya kuanza ukarabati wa zahanati hiyo kuanzia Februari mwaka huu.

“Nilifanya hivyo ili aweze kuweka msukumo kwa Halmashauri itenge fedha za ukarabati upasao kwa zahanati hiyo ili iweze kuanza kutoa huduma mapema Kama ilivyokusudiwa na wafadhili.

Mbali na kufadhili sekta ya afya lakini bado umekuwa ukichangia huduma nyingine kama elimu,” alisema.

Dk. Kikoyo alisema “kwa nguvu uliyonayo tunaomba utusaidie kuanzisha siku ya kumbukumbu ya Ijumbi ‘Ijumbi Day’ karibu na siku za Noeli na mwaka mpya ili iweze kuwakutanisha wazawa wa kata hiyo wanaoishi mkoani Kagera na nje ya Mkoa na nchi za nje ili waweze kuchangia maendeleo ya nyumbani ambako ndiko iliko asili yao,” alisema.

Pia tunaomba utusaidie kuhamasisha wana Ijumbi wengine ambao wanauwezo wa kutoa ajira wawasaidie vijana wa Ijumbi waliohitimu masomo na hawajapata fursa ya ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles