MANCHESTER, England
BAADA ya siku 12 za mateso na kukata tamaa kutokana na lawama alizokuwa anatupiwa na wadau mbalimbali wa soka duniani kutokana na kukutwa amelewa wakati akiwa katika majukumu yake na Timu ya Taifa, mshambuliaji, Wayne Rooney, ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Manchester United katika michuano ya Ulaya.
Rooney ameweka rekodi hiyo baada ya kufunga bao lake la 39 katika michuano ya Ulaya ngazi ya klabu na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Feyenoord ya Uholanzi.
Mabao mengine yalipachikwa kimiani na Juan Mata, Jesse Lingard na kipa Brad Jones wa Feyenoord, aliyejifunga baada ya kuubabatiza mpira uliopigwa na mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic.
Bao zuri lililofungwa na straika huyo mwenye umri wa miaka 31, limeweka rekodi na kumpita mshambuliaji wa zamani, Ruud van Nistelrooy, aliyefunga mabao 38 katika michuano ya Ulaya.
Kwa sasa Rooney anadaiwa bao moja, ili kufikia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote, Sir Bobby Charlton, aliyefunga mabao 249 katika michuano yote, dhidi ya Rooney ambaye mpaka sasa amefunga mabao 248 .
Wachezaji wengine wa Manchester United waliofunga mabao katika michuano ya Ulaya ni Ryan Giggs mabao 29, Denis Law mabao 28 na Paul Scholes aliyefunga mabao 26.
Wengine waliofunga mabao mengi katika michuano yote ni Denis Law -237,
Jack Rowley mabao 211, Dennis Viollet na George Best kwa pamoja walifunga mabao 179.
Nyota wa zamani Old Trafford, Paul Scholes, amempongeza Rooney, akisema: “Kila mmoja ndani ya klabu hiyo anafahamu uwezo wake wa kufunga mabao mengi, ni mafanikio makubwa.
“Amefunga bao zuri na United walistahili kufunga mabao mengi zaidi, yangefika hata sita,” alisema Scholes.
Kwa upande wake Rooney, alisema: “Nina furaha kufunga mabao nikiwa na klabu hii, nimeridhika na ninatarajia mabao mengi zaidi kutoka kwangu.”