Na AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM
WATU wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha.
Waliofikishwa kortini jana ni Hamza Mwaya (25), mkazi wa Mbagala Chamazi na Abdul Mohamed (18) mkazi wa Mbande, ambapo walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa.
Wakisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Neema Moshi, alisema Septemba 15, mwaka huu eneo la Tegeta Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam washtakiwa hao waliiba vifaa vya gari lenye namba za usajili T 371 DMG Toyota vanguard mali ya Aimtonga Amani.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba vifaa walivyoba kwenye gari hiyo ni kioo cha mbele chenye thamani ya Sh milioni tatu, taa za mbele mbili yenye thamani ya Sh milioni mbili, vioo vya madirisha ya gari vyenye thamani ya Sh milioni 1.6 pamoja na Box Memory la thamani ya Sh milioni nne.
Katika shtaka la pili siku hiyo ya tukio washtakiwa hao walitenda kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha na kuiba simu mbili aina ya Tekno zenye thamani ya Sh 80,000 kila moja mali ya Emmanuel Mbimbi na Silveter Kilamulya.
Washtakiwa wamekana kutenda kutenda makosa hayo na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilik.
Kutokana na hali hiyo Hakimu Kiliwa, alisema kesi hiyo haina dhamana na washtakiwa wakupelekwa rumande hadi Desemba 10, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.