29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mfumo mapato ya Serikali wamkuna Gavana BoT

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM


GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa  Florens Luoga, amewapongeza wafanyakazi nane wa benki hiyo upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mchango na uzalendo wa hali ya juu uliowezesha kusimikwa kwa mifumo ya kielektroniki ya kulipa mishahara na kukusanya mapato ya serikali nchini.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi katika hafla fupi ya kuwapongeza wafanyakazi hao kwa kushirikiana na wataalam kutoka taasisi zingine za serikali katika kubuni, kutengeneza na kusimika mifumo ya kukusanya malipo ya serikali kielektroniki ya GePG na kulipa mishahara kupitia Benki Kuu ya Tanzania (GSPP) kati ya mwaka 2015 na 2018.

“Siku zote, Benki Kuu imekuwa ikihamasisha wafanyakazi wake kujituma katika kazi kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu ili kuongeza tija na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

“Katika hili tunawapongeza kwa kuwa mmetekeleza kwa vitendo falsafa hii kutokana na utendaji wenu uliotukuka. Hongereni sana!,” alisema Prof. Luoga.

Alisema kwa kutumia wataalamu wa ndani kusimika mifumo hiyo, sio tu kumeiwezesha serikali kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, bali pia kumeliwezesha taifa kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kununua mifumo kama hiyo kutoka nje ya nchi.

Pamoja na pongezi hizo, Gavana Luoga amewakabidhi wafanyakazi hao barua ya pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, Balozi John Kijazi, aliyoitoa kwao kutokana na kazi yao kutambuliwa na Rais Dk. John  Magufuli wakati taarifa ya kazi hiyo ilipowasilishwa kwake na Wizara ya Fedha na Mipango.

Wafanyakazi waliopongezwa ni kiongozi wa timu ya BoT, Joel Ngussa, Eric Lwambura, Mutashobya Mushumbusi, Jeremiah Tunutu, Mota Cecilia Mlama, Emmanuel Millinga, Anthony Lyaruu na George Sije.

“Aidha, napenda kutoa rai kwa wafanyakazi wote wa Benki Kuu kuchukulia mafanikio ya wenzetu hawa wachache kama chachu katika utendaji wenu wa kazi.

“Heshima ya Taasisi hii katika taifa na hata kimataifa itatokana na jinsi kila mmoja wetu anavyofanya kazi kwa kujituma, kwa weledi na kwa kuleta matokeo chanya ambayo yatasaidia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla,” alisema

Alisema Benki Kuu itaendelea kufanya kazi kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa manufaa ya taifa.

“Ni wajibu wa taasisi hii na taifa kwa ujumla kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wataalam wa ndani kwa kuhakikisha wanatumika kikamilifu,” alisema

Awali Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Kened Nyoni, alisema utekelezaji wa miradi hiyo umeiwezesha serikali kuanza kulipa mishahara ya watumishi wake kupitia Benki Kuu ya Tanzania, kuokoa fedha zilizokuwa zinalipwa kwa mawakala katika mchakato wa ulipaji mishahara pamoja na kuharakisha mchakato mzima wa ulipaji.

Alisema mfumo wa GePG umeiwezesha serikali kukusanya mapato ya taasisi zake kikamilifu, kuwa na uwezo wa kujua kila wakati kiwango cha makusanyo (maduhuri) yake na pia kupunguza upotevu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles