AVELINE KITOMARY Na MARRY NYARI
-DAR ES SALAAM
WATU wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, Dar es Salaam kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha.
Waliofikishwa mahakamani jana ni Mtuli Chacha (29) mkazi wa Pugu Kajiungeni na Said Ramadhani (19) mkazi wa Mwananyamala Kisiwani ambao walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Boniface Lihamwike.
Wakisomewa mashtaka yao, karani wa mahakama hiyo, Ramadhan Kalinga, alidai kuwa Mei 4, mwaka juzi katika eneo la Makumbusho Millennium Tower, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa hao walimtishia kwa panga na bastola William Charles na kumwibia mali yake.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba vifaa walivyoiba ni begi lenye thamani ya Sh 45,000, kompyuta mpakato aina ya HP yenye thamani ya Sh 600,000 na simu aina ya Tekno yenye thamani ya Sh 250,000.
Washtakiwa walikana kutenda kosa hilo, hata hivyo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Kutokana na hali hiyo Hakimu Lihamwike, alisema kesi hiyo haina dhamana na washtakiwa walirudishwa rumande hadi Februari 29, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakati huo huo, Issah Ibrahim (25) mkazi wa Mabibo Farasi amepandishwa kizimbani kwa shtaka la ubakaji.
Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Boniface Lihamwike, karani wa mahakama hiyo, Ramadhani Kalinga alidai kuwa kati ya Mei 2 na Septemba mwaka jana eneo la Mabibo, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, alimbaka msichana wa miaka 16 jina tunalo.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo, hata hivyo upande wa Jamhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na aliachiwa kwa dhamana hadi hapo kesi yake itakaposomwa tena Februari 29.