24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yatua Kinshasa kuiwinda AS Vita

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Simba jana kimewasili salama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kikisubiri kuivaa AS Vita katika mchezo wa hatua ya makundi  ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa kesho jijini Kinshasa.

Kikosi cha Simba kiliondoka jana kwenda DRC kikiwa na wacheza 20, pamoja na viongozi kadhaa wa utawala na benchi la ufundi ambalo linaongozwa na kocha mkuu, Patrick Aussem.

Wekundu hao wa Msimbazi wataivaa AS Vita wakiwa na kumbukumbu ya kuinyuka JS Saoura ya Algeria mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya mchezo wake wa kesho kutarajiwa kuwa mgumu, mashabiki wa timu hiyo wana imani na kikosi chao kwamba kina uwezo wa kushinda  ugenini.

Matumaini hayo yanatokana na kasi ya washambuliaji wa timu hiyo katika kupachika mabao.

Safu ya ushambuliaji ya Simba imekuwa ikiongozwa na Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco, ambaye hataambatana na timu kutokana na kuwa majeruhi.

Aussems, ameweka wazi kuwa hana sababu ya kucheza soka la kujilinda, wakati ana kikosi chenye washambuliaji wakali ingawa pia sehemu ya kiungo cha timu hiyo imeonekana imara kwani Jonas Mkude, James Kotei na Clatous Chama, wamekuwa wakitakata.


“Nafahamu mchezo utakuwa mgumu kutokana na uwezo wa wapinzani wetu ambao tunaenda kukutana nao, hata hivyo nimekiandaa kikosi changu kwa ajili ya kushambulia ili kupata mabao na hatimaye ushindi,” alisema.

Alisema mara nyingi mechi za ugenini zinakuwa na ushindani, lakini ushindi walioupata kwenye mechi zilizopita umewapa morali ya kuendelea kufanya vizuri.

Simba ipo Kundi D pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DRC na JS Saoura ya Algeria.

Miamba  hiyo ya soka yenye makao yake Msimbazi jijini Dar es Salaam, inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi tatu, sawa na Al Ahly iliyoko nafasi ya pili kutokana na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, AS Vita katika nafasi ya tatu na JS Saoura ikikamata mkia, zote zikiwa haina pointi yoyote.

Simba ilitinga hatua ya makundi baada ya kuitoa mashindanoni Nkana FC ya Zambia kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-3, ikianza kuchapwa mabao 2-1 mjini Kitwe, kabla ya kushinda mabao 3-1 nyumbani, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles