NA ALOYCE NDELEIO
NI jambo la kushangaza kuwa baada ya wawekezaji kuona kuwa baada ya kuiingiza Serikali katika mtego wa mikataba ya kinyonyaji kazi yao kubwa ilikuwa ni kuIsifia Serika kwamba kile walichokifanya kilikuwa ni sahihi.
Ukweli ulibakia kwamba kampuni za madini zilikuwa zinaona wazi au kwa kutumia hila au rushwa kuwa mikataba hiyo haikuwa sahihi na walikuwa wanakenua kwa kufanikiwa katika ulaghai.
Hali hiyo ndivyo ilivyokuwa miongoni mwa kampuni za madini zilizowekeza nchini na miongoni mwake ikiwa ni Kampuni ya Barrick Gold Tanzania Limited kwamba ilikanusha tuhuma kuhusu mkataba wa mgodi wa Buzwagi kwa kusema kwamba ni tuhuma za vyama vya upinzani na si za kweli.
Barrick ilisema Agosti 2007 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, kwamba mkataba huo baina ya Barrick Gold na Waziri ya Nishati na Madini wa wakati huo, Nazir Karamagi jijini London, ulipitishwa katika ngazi zote muhimu za Serikali ya Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Barrick, Deo Mwanyika, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mkataba ulisainiwa haraka kupunguza gharama za muda na pesa.
Mwanyika alisema Barrick iliiambia Wizara ya Nishati na Madini kwamba mkataba huo ulitakiwa kutiwa saini mapema ili kuwahi shughuli muhimu za kifedha na uzalishaji.
Aliongeza kusema kwamba masuala kama ya urari na uwekezaji mbadala yangeweza kuathiri sana matokeo ya mradi huo kama utiaji sahihi mkataba ungecheleweshwa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa Barrick, kampuni anayoongoza ilishafanya vikao vingi na watendaji wa Serikali wakiwamo wataalamu kadhaa walioteuliwa na Wizara ya Nishati na Madini kabla ya kufikia mkataba huo.
“Kulikuwa na mazungumzo na majadiliano marefu kwa miezi minane ambapo tulitakiwa kuwasilisha taarifa za kina kuhusu mradi huo kwa timu ya Serikali inayoshauri masuala ya madini,” alifafanua.
Mwanyika alisema baada ya makubaliano kufikiwa Barrick iliarifiwa kwamba mkataba utatiwa sahihi Februari 16, 2007, na kwamba masuala yote muhimu kuhusu leseni yalikuwa yamekamilishwa na Serikali.
“Hapo ndipo tulipokamilisha taratibu za ndani za kifedha na sahihi za kifedha. Tulipata pia kibali cha Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),” alisema.
Februari 15, 2007, siku moja kabla ya kusainiwa kwa mkataba, Barrick Gold waliarifiwa kwamba shughuli hiyo imeahirishwa kwa sababu Waziri Karamagi alikuwa nje ya nchi na hatarudi hadi baada ya wiki mbili, alisema.
Hatimaye Barrick Gold waliarifiwa kwamba utiaji sahihi utafanywa jijini London na hivyo ujumbe wa Barrick ukasafiri hadi London na kutia sahihi Februari 17, 2007.
Kwa mujibu wa Mwanyika mkataba ulitiwa sahihi mbele ya Balozi wa Tanzania Uingereza.
Mradi unatarajiwa kutoa wakia kati ya 250,000 hadi 260,000 za dhahabu katika miaka mitano ya awali. Buzwagi kuna dhahabu ya wakia milioni 2.64.
Mwanyika alisema eti hata hivyo hakuna mwekezaji angekuja kwa sababu dhahabu iliyopo ardhini imetapakaa mno na hivyo tani moja ya udongo hutoa wakia mbili tu za dhahabu.
Alifananisha mgodi unaohitaji mtaji wa Dola za Marekani milioni 400 na Mgodi wa Bulyanhulu unaohitaji mtaji wa Dola milioni 280 kupata wakia milioni 10 kuwa una hadhi ndogo kiuchumi.
Mkataba wa Mgodi wa Buzwagi ulifumua mjadala mkali bungeni na kusababisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakati akiwa (Chadema) kuomba Bunge liunde kamati maalumu ya uchunguzi..
Kilichotokea baadaye ni Kabwe aliishia kufungiwa ubunge kwa miezi sita na hoja yake kutupiliwa mbali kutokana na upinzani na wingi wa wabunge wa CCM bungeni.
Hali hiyo inaonesha kuwa kile kinachotokea hivi sasa katika sekta hiyo ya madini na mijadala inayochangiwa na wabunge ndani ni kwamba ule uliokuwa unaelezwa kuwa ni uongo umebadilika kuwa ukweli ikiwa ni miaka kumi baadae.