Luqman Maloto
UNAPOTAKA kukabiliana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, weka akilini kuwa unawindana na watu wenye akili nyingi, vilevile hutumia wasomi wabobezi wa teknolojia ili kujihakikishia usalama kila siku.
Wana akili nyingi, maana kadiri mamlaka za nchi mbalimbali hasa mataifa makubwa kama Marekani, China, Uingereza na kadhalika, yanapobaini mbinu mpya, tayari wauza dawa za kulevya wanakuwa na mbinu tofauti.
Mbinu hizo ni zile za kimawasiliano ili wasije kubainika, vilevile mbinu za usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka nchi moja kwenda nyingine. Kote huko wanatumia teknolojia ya hali ya juu.
MAWASILIANO
Wauza unga wana fedha na kadiri magenge ya wauza unga yanavyotengeneza fedha nyingi ndivyo wahusika wanavyowekeza zaidi kuhakikisha wanaendelea kufanikiwa katika biashara hiyo haramu.
Hatua waliyofikia kwa sasa, huajiri wataalamu wa kiwango cha juu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambao huwatumia kutengeneza programu za simu (application) zenye kuzuia simu kutoingiliwa wala mawasiliano yake kuonwa na mtu wa tatu.
Mathalan; ukiwa na simu aina ya android kisha ukapakua hiyo application, maana yake simu yako haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote. Mamlaka za serikali zikitaka kuifuatilia simu yako unawasiliana na akina nani zinaambulia patupu.
Application hizo huwa kikwazo mpaka kwa wataoa huduma kuona hasa mteja wao anawasiliana wapi na nani. Mradi simu inakuwa imewekewa muda wa maongezi, mtu anampigia yeyote na kumtumia ujumbe amtakaye pasipo kubainika.
Hizo application huwa zina programu zenye kuweka zuio kwa mtu wa tatu kubaini mawasiliano ya mteja, yaani end to end encryption. Hivyo, mawasiliano yanakuwa kwa wale wanaowasiliana tu. Wauza unga hutumia hivyo kwa faida zao.
Mathalan, ipo application inaitwa telegram ambayo mtu mwenye simu ya android akiipakua na kuhifadhi, inamwezesha kutuma ujumbe wa kawaida (normal text message) ambao utaonwa kati ya mtumaji na yule anayetumiwa tu.
Vilevile hutumia mtandao wa WhatsApp ambao pia hulindwa na programu ya end to end encryption, ingawa huwa na hofu kuwa wamiliki wa WhatsApp wanaweza kuvujisha siri zao. Kwa kawaida program ya end to end encryption humzuia hata mtoa huduma kuona mawasiliano ya mteja wake.
Wauza unga pia hutumia mawasiliano ya alama na namba. Mfano muuza unga anampigia simu mteja wake, anamwambia ‘24 17 87’ kisha anayepigiwa naye anajibu ‘09 24 60’, mpaka hapo wao wanakuwa wameshaelewana. Hivyo, wanakutana na biashara inafanyika.
Wengine hutumia simu za vibandani (call box) kisha kutumia kitambaa ambacho huzuia sauti ya mhusika isitoke kwa uhalisia anapowasiliana na muuza unga. Hii husababisha polisi wanapomkamata wapate shida kumtia hatiani, maana sauti aliyosikika akipiga simu haifanani na inayosikika kwenye rekodi.
Njia za mawasiliano ambazo wauza unga huzitumia, hubadilika kulingana na wakati, jinsi wanavyoshitukiwa pamoja na mazigira ya kiusalama ya nchi husika. Katika nchi ambazo teknolojia ya mawasiliano ipo chini, wauza unga huwasiliana bila hofu, ingawa tahadhari ni lazima.
USAFIRISHAJI
Ubunifu wa kutumia vitunguu, kuvikata katikati na kujaza dawa za kulevya ni wa kienyeji mno, wauza unga wapo makini na hutangulia mbele kiteknolijia.
Matumizi ya matumbo bandia ya mimba (fake pregnant belly) unachukua kasi. Unamwona mwanamke mjamzito, nawe unaamini ana mtoto tumboni kumbe lile tumbo limehifadhi dawa za kulevya.
Fake pregnant belly unaenda sambamba na kumeza kete ambao kwa Tanzania vijana wengi wanaoitwa mapunda, hutumiwa kwa ajili ya kusafirisha dawa za kulevya, japo hatari yake ni kubwa.
Njia hiyo ya kumeza kete, mmezaji akishafika eneo la tukio huzitoa kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, hatari yake ni kuwa kete zikikaa muda mrefu mmezaji hupata madhara ya kiafya hata kubainika haraka.
Na kwa hali ya sasa, mtu akishapata mabadiliko ya kiafya kwenye ndege au akiwa uwanja wa ndege, wakaguzi humshuku kuwa amebeba unga, hivyo kumfanyia vipimo. Hata kama anaumwa malaria, hisia namba moja huwa ni kuwa mtu husika amezidiwa na unga.
Zipo chupi maalum za kike na za kiume kwa ajili ya kusafirishia unga. Wanaume wana suruali yenye mifuko kwa ndani. Kimsingi njia ni nyingi na si rahisi kujua anayetokeza amekuja na mbinu gani.
Magenge ya wauza unga hutengenezesha magari maalum ya kusafirishia unga. Unaweza kulisimamisha na kulikagua kila mahali na usione unga.
Mfano wewe unaona gari ni Toyota Rav4. Watu wanajua Rav4 zilivyo. Wewe unakagua ndani kisha huoni kitu. Wenye gari lao wakifika mahali panapohusika, bodi la nyuma linavutwa, Rav4 inakuwa na mwonekano wa Pickup. Katikati kunakuwa eneo lenye kubeba hata Kg 300 za cocaine.
Tukokotoe sasa. Gram moja ya cocaine katika soko la dunia kwa bei ya kutupa ni dola 200, yaani Sh 447,000. Kwa msingi huo, kg moja ya cocaine ni dola 200,000, Sh 447 milioni. Kg 300, maana yake ni Sh 134 bilioni.
Mtu ambaye anatengeneza Sh134 bilioni kwa mkupuo mmoja, anapoingiza magari 10 hatari yake ni kiasi gani? Magari hayo hupita mipakani na mengine hupokelewa bandarini na kulipiwa kodi na ushuru. Wakaguzi hawawezi kujua magari yamebeba nini. Wakiangalia dani yapo tupu.
Magari mengine yanatengenezwa kwa aina yake. Yale maeneo yenye power windows na chini ya viti yanafunguliwa kwa batons (vitufe). Sehemu moja ya power window inaweza kuwekwa mpaka kg 20 za cocaine.
Askari akiangalia, akivuta power window hazifunguki na kila eneo lipo sahihi, ila wenye magari yao wanabonyeza vitufe panaachia kisha mzigo unatolewa.
Wauza unga wanamiliki viwanda bubu na vingine halali. Unakuta makontena ya kondomu yanasafirishwa kwa sababu za kibiashara au misaada. Kagua kondomu imefungwa vizuri kwenye pakti yake. Kumbe ndani kondomu zimejazwa heroin.
Unga unasafirishwa kwa vinywaji vya kopo. Utakuta kinywaji na utafungua unywe kuhakikisha. Kumbe lile kopo limegawanywa katikati, juu kinywaji, chini unga. Hiyo ni kazi ambayo inafanyika kiwandani. Wahandisi wenye utaalamu wa hali ya juu huifanya hiyo kazi.
Wauza unga hutumia mpaka magari ya jeshi kwenye baadhi ya serikali. Gari linakuwa na matenki hewa ya mafuta yenye kutumika kuhifadhi unga. Maboti, meli na kadhalika, pia hutengenezwa kwa muundo maalum wenye kuwezesha usafirishaji wa unga.
Brian O'Dea, raia wa Uingereza, alikuwa bilionea wa unga kabla hajaacha. Katika kitabu chake kinachoitwa ‘High: Confessions of a Pot Smuggler’, kilichotoka Aprili 11, 2006, anaeleza kuwa alifanikiwa kuifanya biashara hiyo kwa mafanikio kwa sababu haikuwa rahisi kumkamata.
O’Dea ambaye aliwahi kufungwa Marekani miaka 10, anaandika kuwa wakati fulani baada ya kutoka jela hakuwa na fedha, hivyo alikwenda Colombia na kujitambulisha kwenye genge la Sinaloa, linaloongozwa na ‘mtu mbaya’, Joaquin Guzman ‘El Chapo’ kuwa naye ni memba ila alikuwa jela.
Huko alipewa gram 50 tu za cocaine ambazo alipita nazo sehemu zote za ukaguzi lakini wakaguzi hawakugundua alibeba unga kwa sababu walimuona ameshika pakti ya sigara. Naye kuwapoteza aliifungua kabisa na kutoa sigara moja na kuvuta.
Kwamba unaona pakti ya sigara, unafungua unakuta sigara zenyewe lakini ndani watu wamefunga mzigo kati ya gram 50 mpaka 100.
O’Dea anasema pia kuwa alinunua meli ya uvuvi ambayo aliitumia kusafiri na kuuza unga ndani ya bahari ya Pacific. Wakaguzi walipoiona walikagua na kukuta samaki, lakini ndani kulikuwa na cocaine.
Anasema samaki hao walipakiwa kwenye malori na kupita barabarani wakiwa wamewekewa barafu kama vile wanaenda kuuzwa, lakini walipofika sehemu husika walitoa unga ndani ya samaki kisha biashara kubwa ilifanyika.
Kwa leo tuishie hapa, tukutane Alhamisi ijayo tuone jinsi ambavyo biashara ya dawa za kulevya inaweza kumfanya mtu atoke sifuri hadi kumiliki fedha Sh 2.23 bilioni ndani ya miezi miwili.
Luqman Maloto ni mchambuzi na mshauri wa siasa, jamii na sanaa. Tovuti yake ni www.luqmanmaloto.com ambayo ni maarufu kama Maandishi Genius.