23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

KUFICHA MAKOSA YAKO NI SABABU YA KUKUZIDISHIA HUZUNI

Na Christian Bwaya


DAUDI yuko kwenye wakati mgumu. Wasiompenda wanadai wana ushahidi kuwa anatumia jina lisilo lake. Amenunua cheti cha mtu mwingine. Mambo yalipokuwa magumu shuleni alifanya mipango ya kuomba cheti cha mtu mwingine kumwezesha kuendelea na masomo yake.

Wakati huo Daudi akiitwa Albert hakuona shida. Kuomba jina la mtu mwingine kulimsaidia kufikia malengo yake. Kulimjengea heshima. Albert akasoma kwa jina la Daudi akafaulu masomo yake. Akapata kazi. 

Miaka kadhaa baadae, yanaibuka madai kuwa kijana anayefahamika kama Daudi kimsingi ni Albert. Madai haya si tu yanamchanganya Daudi, hata wanaomfahamu kwa jina la Daudi hawajui wamsaidieje. Mwenyewe anafahamu fika kuwa yeye ni Albert. Lakini afanyaje wakati huu ambapo kila mtu anamtambua kama Daudi? Aikubali aibu hii na kukubali kuwa yeye ni Albert mwenye sura ya Daudi? Akifanya hivyo si itakuwa sherehe kwa wabaya wake? Kwani kuwapa wabaya wake kicheko?

Daudi anakosa amani. Hapati usingizi. Hajui afanye nini katika mazingira haya. Nafsini mwake hana hakika kama anachotakiwa kukifanya ni kujilaumu kwa kosa la kutumia jina la mtu mwingine au kuendelea kuuficha ukweli anaoujua. 

Juma lililopita tulipendekeza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kutokujilaumu kwa magumu yasiyobadilika. Ndivyo tunavyoweza kumshauri Daudi. Badala ya kufikiria yaliyopita, anahitaji kuchukua hatua na kukubali makosa yake. Furaha hutegemea na vile tunavyokuwa wepesi kukubali makosa hata yale yanayotudhalilisha. 

Mara nyingi tunapokuwa kwenye nyakati ngumu kama hizi anazokabiliana nazo Daudi, tunajitahidi kufikiri namna ya kuficha makosa yetu. Tunafanya hivyo kulinda heshima na hadhi tunazoamini tunazo. Tunafanya kila linalowezekana kuficha makosa yanayoweza kubomoa ‘brand’ zetu. Tunachosahau, hata hivyo, ni kuwa jitihada za kuyaficha makosa yetu zinakwenda sambamba na kujinunulia huzuni. Daudi anahitaji kujenga ujasiri wa kukabiliana na ukweli unaomwumiza bila kujali gharama za kufanya hivyo. Huko ndiko kujitambua.  

Katika hali ya kawaida, wengi tunapojikuta katika mazingira kama haya, tunakuwa wepesi kutafuta sababu. Badala ya kukabiliana na ‘mazimwi’ haya, tunajaribu kuonesha kwanini wanaozungumzia ‘mazimwi’ yetu wanaoongozwa na chuki.

Kila mmoja ana ‘zimwi’ lake asilopenda lifahamike. Kuna wanaoficha wapenzi wao wa zamani. Hawapendi wapenzi hao wafahamike kwa hofu ya kupoteza heshima walizonazo. Anapotokea mtu anayejaribu kuamsha ‘zimwi’ tunalolificha amani yetu inapotea.

Wapo wanaoficha vipande vya historia ya maisha yao wasivyovipenda. Pengine ni kutoa mimba. Pengine ni kupata mtoto asiyetarajiwa. Pengine ni kufeli mitihani. Pengine ni kuachika. Hayo ni mazimwi tunayoweza kutumia nguvu nyingi kuyadhibiti yasifahamike. Tunayaficha mazimwi hayo kwa lengo la kujenga taswira njema. Tunalinda heshima zetu.

Suluhu si kuficha ‘mazimwi’ hayo yasiyopendeza masikioni mwa watu. Suluhu si kutafuta sababu nzuri ya kufafanua kwa nini wanaofukua ‘mazimwi’ hayo wanafanya hivyo. Kufanya hivyo hakuwezi kutusaidia kuwa watu wenye furaha. 

Suluhu ni kuwa na ujasiri wa kukabiliana na vipande vya historia zetu visivyopendeza bila kujali hadhi zetu kama wanadamu. Badala ya kufumba macho kukwepa aibu ya kuwa uchi, tufumbue macho bila hofu ya kudhalilika.

Kama tulivyotangulia kusema juma lililopita, furaha yako kwenye kipindi kigumu haitegemei namna gani unajitetea na makosa unayojua umeyafanya. Kinyume chake ndio ukweli. Utayari wa kukabiliana na makosa kwa moyo mkunjufu kutakuhakikishia furaha yako.

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles