Walter Mguluchuma – Mpanda
KUNDI kubwa la wananchi wakiwamo waumini, wamevamia na kushambulia kwa mawe nyumba ya Mchungaji wa Kanisa la Sauti ya Uzima, Nabii Elia (36) wakimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Jina kamili la Nabii Elia limeelezwa kuwa ni Elia Zabron Balashika raia wa Burundi ambaye amekuwa akitoa huduma ya roho zaidi ya miaka sita eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema tukio hilo lilitokea Mtaa wa Kazima Ringini Manispaa ya Mpanda, baada ya waumini kuvamia nyumbani kwa kiongozi huyo.
Alisema waumini watano wametiwa mbaroni na watu kadhaa kutokana na kujichukulia sheria mkononi.
Aliwataja waumini waliokamatwa kuwa ni William Kaluzi (19) mkazi wa Mtaa wa Nsemulwa , Steven Alfred (31) mkazi wa Mtaa Kazima, Nicholaus Shadrack (33) mkazi wa Mtaa wa Kazima na Tekla Didas (17) mkazi wa Kijiji cha Rungwa
Wengine ambao siyo waumini wa kanisa hilo ni Mashaka Moshi (23) mkazi wa Mtaa wa Nsemulwa na Faraja Hussein (22) mkazi wa Mtaa wa Kazima.
Kamanda Nyanda alisema chanzo ni imani za ushirikina baada ya taarifa kuzagaa kuwa Nabia Elia alikuwa ameweka ‘misukule’ watano nyumbani kwake ambao waumini wa kanisa hilo walimtaka awatoe hadharani.
Alisema siku ya tukio saa 11:30 jioni, Nabii Elia alifka Kituo cha Polisi mjini Mpanda ambako alitoa taarifa kuwa nyumba yake ilikuwa imevamiwa na wananchi ambao walikuwa wanaharibu mali zake .
“Ndipo timu ya polisi wakiongozwa na SSP Focus Malengo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Katavi, Abdallah Hussein na Kaimu Ofisa Upelelezi Wilaya ya Mpanda, Mkaguzi Ngagala, walifika eneo la tukio na kukuta kundi la wananachi wakiendelea kurusha mawe,“ alieleza.
Alisema walianza kutuliza ghasia kwa kufyatua mabomu ya kishindo kuwatawanya wananchi hao, huku waumini wawili wa kanisa hilo wakijeruhiwa kwa kupigwa mawe kichwani .
Waliojeruhiwa ni Mchungaji wa Kanisa hilo, Mussa Elia (24) na mkazi wa Mtaa wa Kazima, Joseph Elia (29) ambao wanadaiwa kuwa ni ndugu zake na Nabii Elia .
Alisema mali za Nabii Elia zilizoharibiwa ni pamoja na vioo vinne vya madirisha ya nyumba yake, kioo cha nyuma cha gari lake la Spacio, huku thamani kamili haijafamika.