27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Munuo awanyooshea kidole madaktari kuharibu ushahidi

*Adai fomu ya PF3 ina kasoro nyingi

Na Mwandishi Wetu



JAJI mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Eusebia Munuo, amesema kesi nyingi za ubakaji zinakosa ushahidi kutokana na baadhi ya madaktari kuandika maelezo ya uongo kuharibu ushahidi baada ya kupewa rushwa na watuhumiwa wa vitendo hivyo.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kuendesha   mahakama ya mfano (Moot court),   kwenye Chuo cha Sheria,  Dar es Salaam.

Mahakama hiyo ya mfano iliendeshwa na kuratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF), kama sehemu ya shamrashamra za kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa  jinsia  zilizozinduliwa mjini Dodoma wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mahakama kama hizo za mfano zinazosimamiwa na majaji watano, zinafanyika pia  mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma kwa kuhusisha kesi za kubuni kama sehemu ya kuelimisha umma kufuata sheria.

Alisema washtakiwa wengi wa kesi za ubakaji wanashindwa kutiwa hatiani kutokana na ushahidi kupindishwa na watu wanaopokea rushwa wakiwamo baadhi ya madaktari wa hospitali mbalimbali.

“Bado watu wanaendelea kula rushwa ndiyo maana kesi nyingi zimekosa ushahidi… utakuta daktari anaandika maelezo ya uongo kwa sababu kahongwa.

“Sasa inakuwa kazi ngumu kufanya uamuzi kesi inapokuwa mahakamani, hatufanyi kazi kwa hisia tunaangalia ushahidi,” alisema.

Alisema alipokuwa anafanya uamuzi  hakuwa akiangalia sifa ya mtu, cheo au umaarufu wake bali sheria na ushahidi unaowasilishwa mahakamani na upande wa mshtaka na utetezi.

“Eti huyu cheo chake ni kikubwa au huyu ni daktari bingwa, ametibu watu wengi haina maana sana kwenye kutoa uamuzi, kinachotakiwa ni kutoa haki.

“Jaji hutakiwi kuangalia huyu ni nani unachopaswa kuangalia ni sheria,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi wanapofanya kazi zao wazingatie maadili na siyo kujadili fedha  kwa sababu  hazitawasaidia,  mwisho wa siku kitu muhimu zaidi ni kwa mhusika kupata haki yake.

Alisema hata kwenye fomu namba tatu ya polisi maarufu kama PF3,  imekuwa na upungufu wa vitu vingi, lakini majaji na mahakimu inawalazimu kujiongeza na kufuatilia vitu vingine  waweze kutoa uamuzi   sahihi.

Alisema kumekuwa na ugumu kwa wanawake wengi kujitokeza hadharani na kushtaki kuwa amebakwa kutokana na tendo lenyewe kuwa la kuaibisha.

“Unaposema umebakwa jamii nzima inakuwa na mawazo tofauti   kuhusu wewe na hata kama una mchumba unaweza kumkosa kwa sababu tu amesikia kwamba uliwahi kubakwa ndiyo sababu wanaamua kukaa kimpya,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya, alisema wameandaa mahakama za mfano kama hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatilii wa  jinsia dhidi ya wanawake na watoto na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na sheria hasa katika makosa ya aina hiyo.

Alisema rushwa ya ngono hasa kwa wanawake nchini bado ni changamoto kubwa   lakini ushahidi nao limekuwa tatizo kubwa ikizingatiwa  baadhi ya wahusika wa vitendo hivyo huharibu ushahidi ili kujinasua wasitiwe hatiani.

“Ushahidi wake ni mgumu, hivi vitu vinafanyika kwa siri kwa hiyo kwenda kutoa ushahidi wake ni vigumu. “Unakuta wanaohusika ni watu wakubwa wenye mamlaka, watu wenye majina makubwa kwenye jamii, kunakuwa na njia nyingi za kuharibu ushahidi,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo kuna haja kubwa ya kuchukua hatua.

Alimshukuru Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  Dk. Vicensia Shule  kutoka na kuzungumza kwa uwazi kuhusu tatizo hilo la rushwa ya ngono   hatua ziweze kuchukuliwa.

“Yeye ni mhadhiri ameonyesha ujasiri, tunaomba mamlaka zimsikilize, zichunguze na zichukue hatua maana mpaka mtu kujitokeza hadharani na kusema kuna rushwa ya ngono.

“Lazima tumpongeze na tukubali kuangalia hili tatizo kama lipo tunafanyeje,” alisema.

Alisema katika siku 16 za kupinga ukatili wa  jinsia waliamua kuandaa mahakama za mfano  kuonyesha mahakama inalichukulia vipi tatizo hilo na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

“Kama nchi tuanze kukemea na kuchukua hatua kuhakikisha tumetokomeza rushwa ya ngono,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles