25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wauaji wa wanawake Arusha mbaroni

Arusha Town
Arusha Town

ELIYA MBONEA NA EDITHA EDWARD, ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limewatia mbaroni watu saba wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya wanawake pamoja na uporaji wa kutumia silaha mjini hapa.

Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, ilisema kuwa kati ya watuhumiwa hao, wawili walifikishwa mahakamani juzi na kusomewa mashtaka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliokamatwa wanahusika pia na tukio la kumpiga risasi mtoto wa miaka mitatu, Christen Nickson, aliyeuawa wakati akiwazuia wahalifu hao wasipore gari la wazazi wake, Agosti 21, mwaka huu.

Kamanda Sabas aliwataja watuhumiwa waliofikishwa mahakamani juzi kuwa ni Japhet Lomnyaki (25), mkazi wa Sakina na Nehemia Kweka (34), mkazi wa Ngaramtoni.

Watuhumiwa wanaoendelea kuhojiwa aliwataja kuwa ni Adam Mussa, maarufu kwa jina la Badi Makonde (30), mkazi wa Majengo, Tito Loomoni (25), mkazi wa Shamsi, Joseph Loomoni (29), mkazi wa Shamsi, Abdallah Maglan (22), mkazi wa Oldadai na Emmanuel Maglan (23), mkazi wa Oldadai.

“Watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika katika tukio la Agosti 21, mwaka huu, lililotokea eneo la Olasite, kwani siku hiyo walikuwa na pikipiki aina ya Toyo na walimjeruhi kwa kumpiga risasi mtoto Nikson na kumuua,” alisema Kamanda Sabas.

Alitaja tukio jingine ambalo watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika kuwa ni la Agosti 6, mwaka huu, lililotokea saa 3:30 usiku maeneo ya Kwa Iddi, wilayani Arumeru.

Wakati wa tukio hilo, Kamanda Sabas alisema watuhumiwa hao walimpiga risasi shingoni Shamimu Rashid (30), ambaye alifariki wakati akipelekwa hospitalini.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sabas alisema Agosti 15, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha liliwakamata watuhumiwa wawili wa ujambazi waliokuwa na bunduki aina ya SMG yenye namba 273888860745.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kursasi Mbotoni (35), mkazi wa Kijiji cha Ng’arwa, wilayani Ngorongoro na Saigulu Migweri.

Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, watuhumiwa hao walikuwa wakijihusisha na utekaji wa vyombo vya moto katika maeneo mbalimbali.

“Hawa watuhumiwa inaonekana waliwahi kuliteka gari lenye namba za usajili T 841 AHC, aina ya Land Rover lililokuwa likiendeshwa na Emmanuel Peter (35), mkazi wa Kilimanjaro.

“Wakati wa tukio hilo, watu wawili walifariki ambao ni Ibrahim Joseph (15), aliyepigwa risasi shingoni na Athuman Hamad, aliyefariki papo hapo baada ya kupigwa risasi.

“Mtuhumiwa Migweri tayari alishafikishwa mahakamani kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na kosa la kukutwa na silaha ya kivita, SMG ikiwa na risasi mbili.

“Alipokuwa mahakamani, alikiri makosa yake na mahakama ikamhukumu kifungo cha miaka 32 jela kwa matukio mbalimbali aliyoyafanya.

“Lakini mtuhumiwa Mbotoni alifariki Agosti 17, mwaka huu akiwa anaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Wasso wilayani Ngorongoro,” alisema Kamanda Sabas.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles