29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishiwa Mahakama watakiwa kuzingatia utunzaj sahihi wa kumbukumbu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

JAJI Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Mohamed Siyani amewataka watumishi wa Mahakama kuzingatia utunzaji sahihi wa kumbukumbu na nyaraka nyingine muhimu kwakuwa Mhimili huo hauwezi kutekeleza majukumu yake bila kuwa na kumbukumbu zinazohifadhiwa vizuri.

Akizungumza Mei 17, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakala wa Usalama wa Afya Mahali pa Kazi (OSHA) jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Jaji Kiongozi Siyani amesema kuwa, Mahakama ina mifumo mbalimbali ya kutunza nyaraka ikiwemo ile ya masjala ambapo nyaraka halisi zinahifadhiwa.

“Sote tunafahamu tuna njia mbalimbali za utunzaji kumbukumbu lakini pia tuna mifumo ya kielekroniki ya usimamizi wa mashauri, najua mnafahamu kuwa tunao mfumo maalumu wa usimamizi wa mashauri (ACMS) ambao umeboreshwa kutoka kwenye mfumo wa JSDS2 tuliouzoea, ni muhimu kila mmoja kuwa na uelewa wa kuutumia,” amesema Jaji Kiongozi Siyani.

Amesema wakati huu ambao Mahakama ipo katika safari ya kuelekea matumizi kamili ya TEHAMA katika utoaji huduma, wanalazimika kuendelea kuhifadhi vema kumbukumbu ikiwemo majalada ya mashauri kwenye masjala.

Aidha, Jaji Kiongozi ameongeza kwamba ana taarifa za kupotea au kutoonekana kwa majalada ya mashauri, ambapo amesema tabia hizo zinazofanywa na watumishi wasio waadilifu iwe kwa makusudi au bahati mbaya ni jambo lisilokubalika na ni uzembe wa hali ya juu ambao haupaswi kupewa nafasi na kufumbiwa macho.”

Jaji kiongozi amewataka watumishi hao pia kubadili fikra hasi ili kuunga mkono maboresho ya utoaji huduma za Mahakama yanayoendelea kufanyika kwakuwa hayawezi kukamilika na kuleta tija inayostahili bila maboresho ya fikra.

“Sote tunafahamu Mahakama imekwishafanya na inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika utoaji wa huduma, ili mafanikio yetu yawe na tija zaidi, ni lazima wafanyakazi wabadilike kwa kila mmoja wetu kuelekeza fikra zake kwenye kutoa huduma bora,” amesema Jaji Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.

Ameongeza kuwa maboresho yanayofanyika hayawezi kukamilika na kuleta tija inayostahili bila kuwa na fikra chanya huku akisisitiza kuwa kila mtumishi ajiulize ni kwa kiasi gani anatoa huduma ambayo kama ikipimwa na watu huru, watakuja na jibu kuwa huduma iliyotolewa ni bora na inaridhisha wateja.

“Ni lazima kila mfanyakazi awajibike kuhakikisha kama tulivyoboresha maeneo mengine, tunaboresha pia eneo hili. Majengo mazuri peke yake bila huduma bora ni bure na huduma bora inatoka kwanza kwa mfanyakazi mmoja mmoja na kisha sote kwa pamoja,” ameeleza Jaji Kiongozi.

Amebainisha kwamba, tafiti zilizofanyika mwaka 2019, zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango cha kuridhika kwa wananchi kwa asilimia 78 kutoka asilimia 61 kwa mwaka 2015, lakini hicho kisiwe kigezo cha watumishi hao kubweteka.

Amewakumbusha pia watumishi hao kuwa na matumizi sahihi ya lugha, uadilifu, muonekano mzuri na mazingira mazuri, kuzingatia muda ili kuwa wepesi wa kutoa huduma kwa wananchi.

“Kuna tatizo la kutoambiana ukweli pale inapotokea kuna ukiukwaji wa maadili, ni lazima tuambiane ukweli. Kuna ugonjwa wa watu kuoneana aibu na hivyo kutowajibishana. Sote tufahamu kuwa, taasisi yoyote ambayo haina uwezo wa kuwajibishana, ni taasisi inayoelekea kuanguka,” amesema Jaji Kiongozi.

Akihitimisha hotuba amewataka wajumbe wa kikao hicho kushiriki kikamilifu kutoa hoja zao, changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ili kupata mwarobaini wa hoja hizo.

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote, Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu sana kinachowaunganisha wafanyakazi na uongozi. Baraza la wafanyakazi ni daraja linalotoa fursa kwa watumishi kupitia wawakilishi wao, kujadiliana na uongozi juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles