22.4 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara waaswa kufuata falsafa ya KAIZEN

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Raslimali watu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Veronica Nchango, amewasisitiza watumishi wa Wizara hiyo kuishi maisha kwa kufuata misingi ya falsafa  ya KAIZEN  inayowahimiza  kuzingatia udhibiti wa mazingira ya kazi na kuboresha usimamizi wa raslimali ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.

Nchango alitoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 1, jijini hapa alipokuwa akifunga mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo ambapo amewataka  watumishi hao kuzingatia ubunifu, ubora na tija ili kupunguza malalamiko, upotevu na gharama zisizokuwa za lazima katika utendaji kazi.

Kaimu  Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Raslimali watu wa wizara ya viwanda na biashara,Veronica Nchango akizungumza wakati akifunga mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo yaliyofanyika katika Chuo cha Biashara CBE jijini Dodoma Mafunzo yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa Wizara hiyo ili kuleta tija mahala pa kazi.

Mkurugenzi huyo aliwataka  watumishi hao kuwa chanzo cha mabadiliko katika utendaji kazi  wao na wawafundishe watumishi wenzao katika wizara nyingine pamoja na familia zao wakiwemo watoto wao ili wakue katika misingi ya kufanya kazi kwa ufanisi, tija na ubora nchini.

Aidha, Mkurugenzi huyo amewashauri wakufunzi wa falsafa ya KAIZEN kuongeza S moja  inayomaanisha “Sensitization”  ili kuhamasisha watu zaidi kujifunza na kutekeleza falsafa hiyo katika kuongeza tija na ubora. “S” nyingine (5) tano  zinazotumika kama njia za utekelezaji wa KAIZEN ni Sasambua (Sort), Seti (Seti), Safisha (Shine), Sanifisha (Standardize) na Shikilia (Sustain).

Mkurugenzi huyo ameshauri  mafunzo hayo yaliyolenga kuongeza ufahamu kuhusu falsafa KAIZEN inayolenga kuongeza thamani endelevu ya tija na ubora viwandani yaingizwe kwenye mitaala ya shule na yafundishwe nchi nzima ili kuhimili kufikia matokeo bora, makubwa na kwa haraka  na kuhimili ushindani.

Pia, amewapongeza watumishi hao kwa kuhudhuria mafunzo hayo pamoja na kutembelea viwanda vinavyotekeleza falsafa ya KAIZEN vilivyopo jijini Dodoma kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.

Alivitaja Viwanda hivyo ni Dane Holding Limited kinachotengeneza mvinyo na kiwanda cha “Groly Farm” kinachozalisha mafuta ya Alizeti.

KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya badilika kwa ubora linalohusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi mifumo michakato na nyanja yoyote ya kuendesha biashara ambapo  asili yake ni Japani lakini sasa inatekelezwa Duniani kote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles