Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Raslimali watu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Veronica Nchango, amewasisitiza watumishi wa Wizara hiyo kuishi maisha kwa kufuata misingi ya falsafa ya KAIZEN inayowahimiza kuzingatia udhibiti wa mazingira ya kazi na kuboresha usimamizi wa raslimali ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Nchango alitoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 1, jijini hapa alipokuwa akifunga mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo ambapo amewataka watumishi hao kuzingatia ubunifu, ubora na tija ili kupunguza malalamiko, upotevu na gharama zisizokuwa za lazima katika utendaji kazi.
Mkurugenzi huyo aliwataka watumishi hao kuwa chanzo cha mabadiliko katika utendaji kazi wao na wawafundishe watumishi wenzao katika wizara nyingine pamoja na familia zao wakiwemo watoto wao ili wakue katika misingi ya kufanya kazi kwa ufanisi, tija na ubora nchini.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewashauri wakufunzi wa falsafa ya KAIZEN kuongeza S moja inayomaanisha “Sensitization” ili kuhamasisha watu zaidi kujifunza na kutekeleza falsafa hiyo katika kuongeza tija na ubora. “S” nyingine (5) tano zinazotumika kama njia za utekelezaji wa KAIZEN ni Sasambua (Sort), Seti (Seti), Safisha (Shine), Sanifisha (Standardize) na Shikilia (Sustain).
Mkurugenzi huyo ameshauri mafunzo hayo yaliyolenga kuongeza ufahamu kuhusu falsafa KAIZEN inayolenga kuongeza thamani endelevu ya tija na ubora viwandani yaingizwe kwenye mitaala ya shule na yafundishwe nchi nzima ili kuhimili kufikia matokeo bora, makubwa na kwa haraka na kuhimili ushindani.
Pia, amewapongeza watumishi hao kwa kuhudhuria mafunzo hayo pamoja na kutembelea viwanda vinavyotekeleza falsafa ya KAIZEN vilivyopo jijini Dodoma kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
Alivitaja Viwanda hivyo ni Dane Holding Limited kinachotengeneza mvinyo na kiwanda cha “Groly Farm” kinachozalisha mafuta ya Alizeti.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya badilika kwa ubora linalohusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi mifumo michakato na nyanja yoyote ya kuendesha biashara ambapo asili yake ni Japani lakini sasa inatekelezwa Duniani kote.