26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi 2,859 wako kwenye mfumo wa utumishi – Wizara

Na Ramadhan Hassan

HADI  kufikia  Agosti, mwaka jana, kulikuwa na watumishi 2,900 wenye ulemavu wa aina mbalimbali ambao kati yao, 2,859 wamo kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara na 41 wako nje ya mfumo.

Hayo yalielezwa bungeni Dodoma jana  na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakati ikijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM).

Katika swali lake, Mollel  alidai kwa mujibu wa mwongozo wa huduma kwa watumishi wa umma wenye ulemavu, imeelezwa bayana umuhimu wa kukusanya na kutunza takwimu za watu wenye ulemavu katika utumishi wa umma.

Mollel alihoji  hadi kufikia sasa kuna watu wenye ulemavu wangapi kwa kuzingatia aina zao za ulemavu ambao wana ajira katika utumishi wa umma.

“Je, kati ya watumishi hao, ni  wangapi ambao wamepata fursa ya kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za kiuteuzi,” aliuliza.

Ikijibu swali hilo, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ilieleza hadi kufikia  Agosti, mwaka jana kulikuwa na watumishi 2,900 wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Kati ya watumishi 2,859 wenye ulemavu waliopo katika mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara, watumishi 46 wenye ulemavu waliokidhi sifa za msingi wameteuliwa kushika nafasi mbalimbali za kiuteuzi.

Ilisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali mwaka 2005, ilibainika pamoja na mambo mengine haukuwepo utaratibu wa kukusanya na kutunza takwimu za watu wenye ulemavu katika utumishi wa umma.

“Kufuatia changamoto hiyo, mwaka 2012, Serikali iliamua kuingiza kipengele cha kuwatambua watumishi wake wenye ulemavu kwenye mfumo wake wa taarifa za kiutumishi na mishahara na hivyo kuiwezesha kuwa na takwimu sahihi za watumishi wenye ulemavu,” ilieleza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2007, watu wenye ulemavu waliokuwa wameajiriwa katika utumishi wa umma walikuwa 689.

Takwimu hizi zinaonyesha  Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuongeza idadi ya watumishi wenye ulemavu katika utumishi wa umma ili kuwapa nafasi katika ujenzi wa taifa kupitia ajira zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles