- Walimu kulipwa Sh bilioni 16.25, wasiokuwa walimu kulipwa Sh bilioni 27.15
Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA
SERIKALI imeidhinisha jumla ya Sh bilioni 43.39 kwa ajili ya kuwalipa watumishi 27,389 waliokuwa wakiidai.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema malipo hayo yameidhinishwa baada ya uhakiki na majina ya watumishi hao wa umma yanatarajiwa kutangazwa leo.
Pia alisema madai hayo ambayo mengine yamekuwapo karibu miaka 10 iliyopita, yatalipwa kwa mkupuo mmoja pamoja na mshahara wa Februari mwaka huu.
Mpango alisema madeni hayo yalibainika ni halali na yanastahili kulipwa baada ya uhakiki wa watumishi 82,111 waliokuwa wakiidai Serikali.
Akitoa mchanganuo wa jinsi madeni hayo yatakavyolipwa, alisema fedha hizo zitajumuisha Sh bilioni 16.25 kwa walimu 15,919 na Sh bilioni 27.15 kwa watumishi wasiokuwa walimu.
“Madai hayo yanajumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishiwa mishahara.
“Malipo hayo na mengine yana zaidi ya miaka kumi na majina ya walipwaji wote yatatangazwa katika magazeti kuanzia kesho (leo),” alisema.
Mpango alisema Serikali imeokoa jumla ya Sh bilioni 84.22 kutokana na uhakiki huo ikiwamo kuwaondoa katika mfumo wa malipo ya mshahara watumishi hewa, wenye vyeti feki na wasio na sifa.
“Huu ndio umuhimu wa kuhakiki, tumeokoa shilingi bilioni 84.22 na Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii yanayoweza kuisababishia Serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili,” alisema.
Pia alisema hadi kufikia Julai mosi, mwaka jana, Serikali ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya Sh 127,605,128,872.81.
“Kupitia Mfumo wa Taarifa za Utumishi na Mishahara (HCMIS), Serikali ilikuwa inadaiwa kiasi hicho cha fedha hadi kufikia Julai mosi, mwaka jana. Madeni hayo yalikuwa kwa watumishi 82,111 wakiwamo walimu 53,925 waliokuwa wakiidai Serikali shilingi 53,940,514,677.23.
“Huku watumishi wasiokuwa walimu walikuwa ni 28,186 na walikuwa wakiidai Serikali kiasi cha shilingi 73,664,614,195.58 na madai mengine yalikuwa ya kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka jana,” alisema.