WAKAZI wanne wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa mahakamani kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kutaka kukusanya kodi ya Sh milioni 175 kwa kutumia barua ya kughushi kutoka Ikulu.
Washtakiwa watatu kati ya hao walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam na kusomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa kuwa ni mwanafunzi Issa Mohammed (27) ambaye hakuwapo mahakamani kwa sababu amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na mwandishi wa habari, Hamisi Tembo (37).
Washtakiwa wengine, ni Wakati Mungi (51) na mtengeneza mihuri, Nicolaus Obado (32), walisomewa mashtaka 12 yanayowakabili.
Nchimbi alidai shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa Machi 16 na 17 mwaka huu, maeneo yasiyofahamika Manispaa ya Ilala kwa pamoja, walikula njama na watu wengine ambao hawapo mahakamani kutenda kosa la kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi 10 na 17,mwaka huu katika maeneo yasiyofahamika jijini, walijitambulisha kwa nyakati tofauti kwamba ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati si kweli.
“Mheshimiwa hakimu, shtaka la tatu washtakiwa wote, kati ya Machi 10 na 17 mwaka huu, walighushi barua wakionyesha ni halali imetoka Ofisi ya Rais ikielekezwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Usangi Logistics Ltd kuweka Sh milioni 25 kwenye akaunti namba 1801833619 katika Benki ya ABC kwa jina la TRA.HR.Mwenge kwa ajili ya kodi.
“Washtakiwa katika shtaka la nne, wanadaiwa kughushi barua wakionyesha imetoka ofisi ya Rais ikielekeza Mkurugenzi wa Bakhresa kuweka benki ya ABC Sh milioni 25, ikiwa ni punguzo la kodi,”alidai Nchimbi.
Washtakiwa katika shtaka la tano, wanadaiwa kuipeleka barua hiyo inayodaiwa kutoka ofisi ya Rais kwa Mkurugenzi wa IPP Media, wakitaka aweke benki Sh milioni 25, ikiwa ni punguzo la kodi.
Katika shtaka la saba, nane, tisa na kumi, washtakiwa wanadaiwa kupeleka barua hiyo kwa Mkurugenzi wa OIL COM , GAPCO Ltd, Lake Oil Tanzania Ltd na Kampuni ya PUMA Ltd.
Washtakiwa wanadaiwa kupeleka barua kwa wakurugenzi wa kampuni hizo, wakionyesha imetoka ofisi ya Rais, ikielekeza kila kampuni iweke benki ya ABC Sh milioni 25 katika akaunti namba 1801833619 iliyopo kwa jina la TRA.HR.Mwenge, malipo hayo ni punguzo la kodi wakati si kweli.
Wakili wa Serikali alidai shtaka la 11 linamkabili mshtakiwa wa kwanza ambaye hakuwepo mahakamani, mashtaka atasomewa akiwa hospitali, katika hati ya mashtaka anadaiwa kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa Kampuni ya Usangu Logistics Limited.
Akisoma shtaka la mwisho, Nchimbi alidai linawakabili washtakiwa Issa na Hamisi, wanadaiwa Machi 10, mwaka huu katika ofisi za TSN walijipatia Dola 1000 za Marekani kutoka kwa Farough Ahmad maarufu Bagozah kwa kudanganya fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya gharama za ufadhili aliopata Issa nchini Marekani.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upelelezi haujakamilika na upande wa Jamhuri ulipinga washtakiwa kudhaminiwa kwa sababu wanaweza kuvuruga upelelezi.
Hakimu alikubali na aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa wa kwanza atakwenda kusomewa mashtaka yanayomkabili Muhimbili Hospitali.
Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja Issa ni mwanafunzi wa shule gani wala Tembo ni mwandishi wa habari wa chombo gani.