24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAT yaicharukia Serikali

549109997_1280x720MAULI MUYENJWA NA RUTH MKENI,DAR ES SALAAM

RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Billy Haonga ameitaka Serikali ieleze ukweli kuhusu ukosefu wa vifaa tiba na dawa katika hospitali mbalimbali.

Pia ameitaka kueleza namna ya kutatua changamoto nyingine zinazokabili sekta ya afya na si kuaminisha umma kuwa watoa huduma ndiyo tatizo.

Kauli hiyo ameitoa  jijini Dar es Salaam jana,wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio lililotokea juzi lililomhusisha Dk, Dickson Sahihi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, mkoani Mtwara  kupigwa, kudhalilishwa utu kwa kuvuliwa nguo na ndugu wa wagonjwa.

Alisema sekta ya afya ni moja ya sekta zenye matatizo makubwa ya rasilimali watu, vifaa na dawa na mpaka sasa inafanyakazi chini ya asilimia 50 katika maeneo mbalimbali nchini.

“Daktari mmoja, anahudumia wagonjwa kati ya 25,000 hadi 30,000  maeneo ya mjini, kule vijijini ni kati ya 50,000 hadi 100,000 tofauti na mpango wa Shirika la Afya Duniani  (WHO), linataka daktari mmoja kuhudumia wagonjwa wasiozidi 10,000 katika miji inayoendelea ,” alisema Haonga.

Alisema  kwa upande wa dawa hali ni mbaya zaidi, huku  maeneo mengine yakikosa dawa wiki za mwanzo za mwezi na baada ya hapo hazipatikani kabisa.

Kutokana na hali hiyo, ametoa siku 14 kwa Serikali kuchukua hatua stahiki kwa vitendo na kama haitafanya hivyo  chama hicho kitaitisha mkutano mkuu wa dharura kujadili usalama wao.

“Mbali na kupigwa Dk.Dickson, matukio mengine ambayo yametuhuzunisha ni pamoja na kusimamishwa hadharani kwa wafanyakazi madaktari na manesi kutokana na uduni wa huduma unaosababishwa na upungufu na ukosefu wa vifaa tiba.

“Kuzingirwa nyumba ya daktari mkoani Katavi na ndugu wa wagonjwa kwa lengo la kumdhuru, baada ya mgonjwa wao kufariki dunia kwa ukosefu wa dawa na damu, haya yote ni matukio ya kusikitisha,”alisema Haonga.

Juzi Serikali ililaani kitendo cha kupigwa daktari huyo na kuviagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua wahusika wote.

Kauli  hiyo, ilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu.

“Ninawasihi sana wananchi wanaopatiwa huduma katika vituo vyetu vya afya kote nchini, kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kufanya vitendo vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya,” alisema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles