JANETH MUSHI-ARUSHA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na kikosi kazi cha ujangili Kanda ya Ziwa, wamekamata watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na bunduki ya kivita aina ya AK 47 na risasi 12.
Alisema watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa walikamatwa Mei 10 mwaka huu saa saba mchana.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika Kitongoji cha Oloshoo, Kata ya Enguserosambu wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Alisema bunduki hiyo ilipatikana baada ya kikosi hicho kupata taarifa fiche kuwa kuna watu wanne, wawili Watanzania na wawili Wakenya wameonekana maeneo ya mpakani wakiwa wanajipanga kuwinda wanyama katika moja ya mbuga zilizopo nchini.
“Tulifanya msako ambao ulifanikisha kupatikana kwa bunduki moja ya kivita na risasi 12. Wanasadikiwa walikuwa na bunduki mbili za kivita, wengine wamekimbilia Kenya.
“Jeshi la Polisi linawataka wahalifu hao kujisalimisha kituo chochote cha polisi kwani wasipofanya hivyo tutalazimika kutumia nguvu kubwa kuwatafuta ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wanaoendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, nawaomba waendelee kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwafichua wale wenye nia ovu ili kumaliza uhalifu katika mkoa wetu,”alisema