23.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa wa ugaidi waipa mtihani mahakama

ugaidi arusha
Watuhumiwa wa kosa la kukutwa na mabomu wakielekea katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha jana kusomewa mashtaka yanayowakabili.

NA JANETH MUSHI, ARUSHA

WATUHUMIWA 14 wa kesi mbili za kudaiwa kufanya uwakala na kusajili vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab cha nchini Somalia wameomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kutaja wapelelezi wa kesi hizo zinazowakabili.

Watuhumiwa hao pia wameiomba mahakama hiyo iwape dhamana au iwaeleze masharti ya wao kupata dhamana.

Kabla ya kuahirisha tena kesi hiyo Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Arusha, Mustafa Siyani, aliwauliza watuhumiwa hao kama wana jambo lolote, ndipo mmoja wa watuhumiwa aliponyoosha mkono kama ishara ya kueleza dukuduku lake ambapo alitaka kujua kama wanastahili dhamana.

“Mheshimiwa naomba kusomewa majina ya wapelelezi katika kesi hii,” alidai mtuhumiwa huyo.

Hatua hiyo ilisababisha Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Hellen Rwijage kuhoji sababu za watuhumiwa hao kutaka kujua majina ya wapelelezi, akidai kuwa kwa ajili ya usalama wao hakuna haja ya majina hayo kufahamika kwa watuhumiwa hao au ndugu zao.

“Kwanza sijaelewa wapelelezi majina yao yanahitajika kwa sababu gani, kwani kiusalama wa wapelelezi wa shauri hili, siwezi kutaja majina ya wapelelezi, atueleze sababu ya kutaka kujua majina hayo,” alidai Rwijage.

Mtuhumiwa huyo alishindwa kutoa sababu ya msingi mahakamani hapo na kudai kuwa wanataka kujua majina yao ili ikitokea wanakwenda kuwahoji wawe wanawajua kwa majina yao.

“Sifahamu kama kuna sheria inayoitaka mahakama iweke wazi majina ya wapelelezi, lakini shauri litakapokuwa kwenye hatua ya usikilizwaji ni lazima wapelelezi watakuwa miongoni mwa mashahidi, hivyo mtawafahamu,” alisema Siyani.

Mtuhumiwa mwingine akiuliza kwa niaba ya wenzake, aliiomba Mahakama hiyo kufahamu kwa nini hawapewi dhamana na namna gani wanaweza kupata dhamana.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali aliieleza Mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya kuzuia ugaidi, ambapo Sheria hiyo namba 22, ya mwaka 2002 inasema kuwa upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.

“Kwa kuwa Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, siwezi kuwaeleza kama kesi hii inadhaminika au haina mdhamana. Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye uwezo wa kusema hayo.

“Zungumzeni na watu wa magereza kule ili kama mna maombi maalumu myawasilishe kwao, ila pia ndugu zenu kama wanaweza kuwatafutia msaada wa kisheria wanaweza kuwaajiri mawakili, muone kama mtapata uwezekano wa kupata dhamana,” alisema Hakimu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua na kukusudia kuua pamoja na kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab, ambao wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu katika baa ya Arusha Night Park iliyopo jijini hapa na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Waliokuwepo mahakamani hapo jana ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemedi, Hasani Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini na Sudi Nasibu Lusuma.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa Abdallah Maginga hajaweza kufika mahakamani kwa kuwa bado ni mgonjwa na atakapopona atafikishwa mahakamani hapo ili kusomewa mashitaka yanayomkabili.

Katika hatua nyingine, watuhumiwa hao waliiomba mahakama kujua hatma ya mtuhumiwa Abdulkarim Thabit. Rwijage aliieleza mahakama hiyo kuwa atafuatilia taarifa zake, kwani hawafahamu chochote kuhusu mtuhumiwa huyo.

Katika hatua nyingine, Jafari Hassan, anayetuhumiwa kughushi pasi ya kusafiria ambapo alitumia jina lisilokuwa lake, aliiomba mahakama kumpunguzia masharti ya dhamana ili aweze kutoka nje kwa dhamana.

“Kesi yangu inadhaminika, nimeambiwa nilete hati ya kusafiria lakini sina, hivyo toka mwezi uliopita sijaweza kupata dhamana kwa sababu hiyo,” alidai.

“Sikukwambia hilo ni sharti la muhimu ili uweze kupata dhamana, lakini kama una hati lazima uiwasilishe mahakamani, lakini kama huna hati unatakiwa kuleta wadhamini, wakikidhi vigezo ukapata dhamana,” alisema Hakimu Siyani.

Kesi hizo zilizokuwa zimefikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kutokana na upelelezi wake kutokukamilika, zimeahirishwa hadi Agosti 7, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles