28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Watuhumiwa mauaji ya Profesa Mwaikusa waachiwa huru

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru Joseph Machecho na Jackson Zebedayo maarufu kama Wambura, waliokuwa wakituhumiwa kumuua kwa makusudi aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Jwani Mwaikusa na wengine wawili.

Washtakiwa hao waliachiwa mwishoni mwa wiki mbele ya Jaji Sirilius Matupa, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka  kuwasilisha hati  akionyesha kwamba hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, aliwasilisha hatia hiyo kwa niaba ya Jamhuri.

DPP alichukua uamuzi huo baada ya kubaini kwamba kuna makosa  ya ufundi na  maelezo ya mashahidi yaliyotolewa na Jamhuri   baada ya upelelezi kukamilika katika Mahakama ya chini  yanatofautiana na ushahidi uliotolewa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa kesi.

Kutokana na mazingira hayo,  Jaji Matupa aliwaachia huru  washtakiwa. Hata hivyo kifungu hicho kilichowasilishwa na DPP  hakizuii Jamhuri kuwakamata tena washtakiwa na kuwashtaki kwa shitaka hilo hilo.

Washtakiwa wako mahabusu wakisubiri kufikishwa mahakamani wakishtakiwa upya kwa makosa hayo ya mauaji ya kukusudia.

Watuhumiwa wanadaiwa Julai 10,2010 maeneo ya Makonde Salasala, waliwaua kwa makusudi, Profesa Mwaikusa, Gwamaka Masanjara Daudi na  John Mtui.

Washtakiwa inadaiwa waliwaua kwa kuwapiga risasi nyumbani kwao Salasala Barabara ya Makonde nje kidogo ya   Dar es Salaam saa 4.00 usiku,

Profesa Mwaikusa alifikwa na mauti baada ya kufika nyumbani kwake  akiwa na gari lake la Nadia  namba   T 876 BEX, wakati akitoka kwenye shughuli zake. Alivamiwa na watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Katika tukio hilo, wakati Profesa  Mwaikusa akijiandaa kushuka katika gari lake, majambazi hao walimgongea kioo na kumwamru kushuka, lakini alisita, ndipo majambazi hayo yalipomvuta kwa nguvu na kummiminia risasi mwilini.

Baada ya kuona hali hiyo, mpwae Profesa Mwaikusa, Gwamaka Daudi (25), ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi VETA  alikwenda kwa lengo la kumnusuru, ghafla majambazi yakamgeukia na kumpiga risasi mgongoni na kufariki dunia papo hapo.

Baada ya kuwaua ndugu wawili, majambazi hayo yalisogea mbele kidogo na kuona kikundi cha watu ambacho walikitilia shaka kwamba walitaka kupambana nao, ndipo walipompiga risasi  John Mtui (45), ambaye ni mfanyabiashara anayeishi jirani na marehemu Profesa Mwaikusa, aliyekuwa na bastola   ya Revolver namba 87668.

Katika tukio hilo, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Agustino Ramadhan, alisema taifa lilipoteza mtu hodari kwenye taaluma ya sheria.

Marehemu Profesa Mwaikusa wakati wa uhai wake  alikuwa mwenyekiti wa jopo la majaji saba waliosikiliza rufaa ya kesi ya mgombea binafsi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles