Na Ashura Kazinja, Morogoro.
WATU wawili wamekufa katika bwawa la maji la Mindu katika Manispaa ya Morogoro na miili yao kukutwa ikielea pembezoni mwa kingo za bwawa hilo.
Miili hiyo ya mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30, na mwili mwingine ukiwa ni wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 6 hadi 9, huku yote ikishindwa kutambulika na wakazi wa mtaa wa Mindu.
Akizungumzia tukio hilo Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro, Fadhili Makala baada ya uokoaji wa miili hiyo, amesema walipata taarifa ya tukio la miili ya watu kuonekana pembezoni mwa bwawa la mindu saa 12 asubuhi na kufanikiwa kuwaopoa kwa nyakati tofauti na kuikabidhi kwa jeshi la polisi la mkoa.
Naye Mkurugenzi wa bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi, , amesema wamekuwa wakizuia shughuli zote za kibinadamu kufanyika katika bwawa hilo hasa zile zinazohatarisha maisha ya watu na ubora wa maji kutokana na maji hayo kutumiwa na watu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Khamis Bakari na Shabani Maneno wote wakazi wa mtaa wa Mindu wamesema awali kabla ya shughuli za kibinadamu kuzuiliwa kufanyika katika hifadhi ya bwawa hilo hapajawahi kuripotiwa matukio kama hayo na kuiomba serikali kurejesha ulinzi wa eneo la bwawa kwa wananchi.