Na EMMANUEL IBRAHIM,
IDARA ya Uvuvi mkoani Geita imekamata matenga 10 ya samaki wachanga wa thamani ya Sh milioni tatu katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
Samaki hao walikuwa wakiingizwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa, kinyume cha sheria.
Walikamatwa juzi katika operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu.
Samaki hao walikuwa wanasambazwa kwenye masoko ya Nyankumbu, Shilabela na Soko la mjini Geita.
Ofisa Mfawidhi mdhibiti ubora wa samaki na msimamizi wa raslimali za uvuvi, Shafii Kitery alisema samaki hao walikamatwa kunatokana na taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema wananchi hao walieleza kuwapo wafanyabiashara waliokuwa wakivua samaki wachanga chini ya sentimita 50 hivyo ukawekwa mtego na kuwakamata.
“Ninashukuru ushirikiano wa wananchi ambao wametoa taarifa hizi.
“Hii ni hatua endelevu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Mwanza akitaka kupambana na uvuvi haramu na kuwalinda samaki wachanga.
“Masoko yote Geita tutayafanyia uchunguzi na kuhakikisha hawa samaki wachanga hawauzwi.
“Watu wanane tuliowakamata tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria vichukue mkondo wake,” alisema Kitery.