Na Clara Matimo, Mwanza
Jumla ya wananchi milioni 1.6 kati ya milioni 1.8 waliokusudiwa kupata chanjo ya uviko 19 mkoani Mwanza wamepata chanjo kamili ya kujikinga na ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa Oktoba 18, 2022 na Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao cha tathmini ya chanjo ya Uviko 19 na uhuru wa kupata habari kupitia mradi wa Boresha Habari unatekelezwa na Internews kwa ufadhili wa USAID na fhi360 ambao unaratibiwa na klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza(MPC).
Dk. Rutachunzibwa alisema idadi hiyo ni mpaka Oktoba 17, 2022 ambayo ni sawa na asilimia 87 ya lengo ambalo ni kuwachanja chanjo hiyo watu milioni 1.8 hadi ifikapo Desemba 2022.
“Hadi sasa bado watu 200000 tunaimani tunaweza kuvuka lengo na mafanikio haya tumeyapata kutokana na nyie waandishi wa habari kwa kuandika habari sahihi kuhusu chanjo ya uviko 19, taarifa na elimu ambazo mnazitoa kuhusu chanjo ya uviko 19 kupitia vyombo vyenu vya habari zimesaidia sana kuwapa wananchi uelewa na zimewaondolea mitazamo hasi waliokuwa nayo kuhusu chanjo hiyo.
“Lengo la kitaifa ni kuchanja asilimia 70 ya watu wenye sifa ya kupata chanjo hiyo hadi ifikapo Desema 2022 kwa hiyo nawasihi waandishi wa habari endeleeni kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo vyenu ili ambao bado hawajapata chanjo hiyo wapate.
Kwa mujibu wa Dk Rutachunzibwa wilaya inayoongoza mkoani humo kwa kuchanja watu wengi ni Ukerewe ambayo imechanja asilimia 89.4 huku wilaya ya Misungwi ikiwa ya mwisho kwa kuchanja asilimia 74.3.
Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko akitoa mada kuhusu jinsi ya kuripoti habari za chanjo ya uviko 19 na uhuru wa vyomba vya habarai aliwasisitiza waandishi wa habari kuhakikisha wanapoandika habari zao hasa za afya zikiwemo zinazohusu ugonjwa wa Uviko 19 kuhakikisha taarifa hizo zinathibitishwa na wataalamu wenye taaluma ya idara hiyo ili wananchi wapate taarifa sahihi.
“Serikali inatutegemea sana waandishi wa habari kuwafikishia taarifa sahihi wananchi wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya afya, inapotokea jambo jipya baadhi ya wananchi huwa na tabia ya kuzusha wakisema mambo ambayo hawana elimu nayo, nyie wenyewe ni mashahidi wakati chanjo ya Uviko 19 ilipoingia nchini wapotoshaji nao waliibuka.
“Wapo waliosema kwamba mtu ukichanja halafu ukaweka balbu eneo ulilochanja inawaka, huo ni uzushi kabisa nia yao ni kurudisha nyuma jitihada za serikali katika kuzuia na kupambana na ugonjwa huo, jamani kwenye hilo kuna ukweli wowote ? Alihoji na kuongeza.
“Sisi wenyewe tulio wengi tumechanja je tukiweka balbu zinawaka? Kwa hiyo tujitahidi kuhakikisha tunawapa taarifa sahihi wananchi ili wasipotoshwe na watu wachache ambao ni wataalamu wa kuzusha,”alisema Soko.