Na Sheila Katikula, Mwanza
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu 24 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ikiwamo mauaji na kuvunja ofisi za shule za msingi na kuiba vitabu.
Akielezea tukio hilo leo Alhamii Aprili mosi, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema kwa kipindi cha miezi miwili Februari na Machi kwa nyakati tofauti ofisi za shule tatu za msingi Wilayani Kwimba ziligundulika kuvunjwa na vitabu 529 vya mitaala mipya vya masomo mbalimbali kuibwa.
Amesema Jeshi hilo linawashikilia walimu wa shule tatu za Msingi za Igoma, Manguluma na Bujingwa kwa kosa la kula njama za kuiba vitabu na kutengeneza matukio ya kufikirika ya kuvunja ili kufikia uhalisia wa tukio hilo.
Amesema walibaini vitabu hivyo viliibwa na kuuzwa kwa wafanyabiashara wa maduka ya vitabu jijini hapa kwani baada ya mahojiano ya kina walikili na kuhusika na ununuzi wa vitabu hivyo.
“Tunawashikiria Walimu watatu ,Walinzi wanne kwa kupokea Mali za wizi na mtaalamu mmoja Mengi Muheta (43)ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Kishiri aliyekuwa anajihusisha na kufuta alama za serikali inayosema kitabu hiki hakiuzwi,”amesema Muliro.
Hata hivyo ameongeza kuwa Jeshi hilo linawashikiria watu wawili kwa tuhuma za makosa ya mauaji ya mtu mmoja 42 yaliyotokea eneo la Kanyerere kata ya Mkuyuni Wilayani Nyamagana kwa kinachodaiwa wivu wa kimapenzi.
“Pembeni mwa mwili wa marehemu waliandika ujumbe kwenye sakafu uliosomeka kuwa mke wa mtu ni sumu kwani watuhumiwa wanafanyiwa mahojiano ya kina na upelelezi ukikamika watafikishwa mahakamani,”alisema Muliro.
Kamanda amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kufichua  vitendo vya uhalifu  na wahalifu  ili hatua stahiki za kisheria  zichukuliwe.
Hata hivyo amewataka wananchi kuelekea msimu wa sikukuu ya pasaka waendelee kutoa ushirikiano kwa  jeshi hilo sanjari na kuhimalisha usalama Katika mkoa huo.
“Tumejipanga  kuanzia Ijumaa kuu mpaka Jumatatu ya pasaka kuhakikisha ibada zote zinafanyika katika mazingira ya usalama kutakuwa na dori za miguu pikipiki na magari katika maeneo yote ya mjini na visiwani kutakuwa salama,”amesema Muliro