WATOTO waliozaliwa na tatizo la kutoshuka kokwa za korodani wapo katika hatari ya kukosa uwezo wa kuzalisha watoto.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Idara ya Watoto, Zaituni Bokhary alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji wanaotarajia kufanya kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo ili kuzishusha.
Alisema korodani zinapaswa kushuka na kuwa nje ya mwili wa mtoto, lakini wapo wanaozaliwa huku korodani zikiwa bado zimebaki ndani ya miili yao, si vizuri. Hapa Muhimbili kwenye idara yetu, kliniki huwa tunaona kati ya watoto wanne hadi watano kila mwezi waliozaliwa na tatizo hilo,” alisema.
Daktari huyo alisema mtoto aliyezaliwa na tatizo hilo anapaswa kuwahishwa kliniki kwa matibabu kwani iwapo atacheleweshwa anakuwa kwenye hatari ya kushindwa kuzalisha.
“Tatizo la kutoshuka kwa korodani hutokana na sababu nyingi, yaani huwezi kusema moja kwa moja imetokana na nini lakini sababu zinazotajwa kuchangia hali hii ni mjamzito kutokula vyakula bora, kukosa kirutubisho cha madini ya ‘folic acid’ na anaposhindwa kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali,” alisema.