NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
WATOTO wanne wenye umri kati ya miaka 7 na 11, wamefariki dunia baada ya kuteketea kwa moto wakiwa wamefungiwa ndani na dada yao ambaye alikwenda Casino.
Tukio hilo lilitokea Julai 7 usiku katika Mtaa wa Nyerere, mji mdogo wa Kibaigwa uliopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, jana alithibitisha kutokea tukio hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari kwa kueleza kuwa watoto hao waliteketea kwa moto wakiwa wamelala.
Alisema dada wa watoto hao ambaye hakumtaja jina aliwafungia ndani ya nyumba yenye vyumba sita iliyojengwa kwa tofali za udongo ambayo ni mali ya Nelson Mdachi, kisha akaondoka na funguo kwenda Casino.
Alikitaja chanzo cha moto huo kuwa ni kibatari kilichokuwa ndani ya chumba kulipuka na kuchoma godoro wakati watoto hao wakiwa wamelala.
Kamanda Mambosasa aliwataja watoto waliofariki kuwa ni Elizabeth Nelson (11), mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Miembeni, Peter Lema (9), mwanafunzi darasa la tatu wa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Paulo, Samweli Mdachi (7), mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Miembeni na Nase Mgomba (9), mwanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Miembeni.
MAJIRANI WAELEZEA
Majirani waliozungumzia tukio hilo walieleza kuwa watoto hao waliachwa na wazazi wao chini ya uangalizi wa dada yao ambaye aliamua kutoka kwenda Casino usiku na kuwaacha akiwa amefunga mlango kwa nje.
Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la Paulo Sauli, alisema dada wa watoto hao anamfahamu kwa jina la Esther na kwamba anapenda kwenda kwenye kumbi za starehe nyakati za usiku huku akiacha amefungia wadogo zake ndani.
Alizitaja kumbi za starehe anazopenda kwenda kuwa ni Maisha Club na VK zilizopo eneo la Kibaigwa na alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa Esther huwa anakwenda Casino kutafuta wanaume.
“Amekuwa na tabia ya kuwafungia watoto hao na kwenda Casino kutafuta wanaume, sasa wakati tukio hili linatokea alikuwa ameenda kutafuta mabwana, Mungu analipa hapa hapa duniani, ameyaweka wazi madudu yake,” alisema Sauli.
Alisema baba wa watoto hao alikwishafariki dunia na kuacha mke wake anayejishughulisha na kilimo akiwalea watoto hao.
“Mama wa familia hiyo anajishughulisha na kilimo sasa akienda shambani huwa anawaacha watoto wake chini ya uangalizi wa Esther ambaye baada ya tukio hili haijulikani amekimbilia wapi. Hapo kuna watu wengi lakini tumemwangalia hapa msibani hatumuoni,” alisema Sauli.
Naye Denis Luhunga, alisema anamfahamu mama wa watoto hao na kwamba siku ya tukio alikuwa amekwenda kuvuna asali katika shamba lake lililoko Kiteto mkoani Manyara na kuwaacha watoto wake chini ya uangalizi wa Esther.
Alisema mazishi ya watoto hao yalifanyika katika eneo la makaburi ya Amani yaliyopo Kibaigwa.