28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Ma-DED wapya waibua mjadala

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

NA EVANS MAGEGE,

HATUA ya Rais Dk. John Magufuli kuteua wakurugenzi wapya wa halmashauri  za majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137 (DED), imeibua mjadala mwingine kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa mwenendo wa Serikali yake.

Mjadala huo umeibuka tena siku chache baada ya Magufuli kufanya uteuzi wa makatibu tawala wa wilaya za Tanzania Bara huku wafuatiliaji na wachambuzi hao wakihoji vigezo vilivyotumika kuwateua kwa kuwa baadhi yao hawakuwa na uzoefu wa kufanya kazi serikalini kwa kuwa hawakuwahi kuwa watumishi wa umma.

Wafuatiliaji na wachambuzi hao walihoji sifa ambazo mtu anatakiwa kuteuliwa kutumikia nafasi ya DED huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kudai kuwa uteuzi huo umechukua makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kumrahisishia Magufuli na chama chake ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa ndio watakaokuwa wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri na manispaa zao. Kwamba kwa kuwa baadhi ya Ma-DED hao 185 ambao kati yao 65 wa zamani na 120 wapya waliotangazwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe, ni makada wa CCM huku wengine waliangushwa katika mchakato wa kura za maoni za uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa kugombea ubunge wa majimbo akiwamo Wakili Elias Nawela, aliyekuwa nyuma ya Kippi Warioba katika kura hizo za Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam ambaye katika uteuzi huo mpya amepangiwa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe iliyopo mkoani Songwe.

Pia wengine walisema kuwa nafasi za DED ni za kitaaluma zaidi na zinahitaji mtu mwenye uwezo wa hali ya juu katika utawala na uendeshaji wa halmashauri na kitendo cha baadhi ya makada hao kuteuliwa kinaweza kusababisha uendeshaji wa miradi ya maendeleo kuwa mgumu na utoaji wa huduma za kijamii ukashindikana.

Wakati wachambuzi na wafuatiliaji hao wakiibua mjadala huo huku ukibebwa katika taswira ya ushindani wa itikadi za kisiasa, baadhi ya wasomi nao wamekuwa na maoni mbalimbali juu ya uteuzi huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana, alisema mjadala dhidi ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa pamoja na makatibu tawala unatokana na wasiwasi usiokuwa na uhalali.

Profesa Bana alisema jambo la msingi katika mjadala huo ni kufahamu wateuliwa wanatoka wapi na walikuwa wanafanya kazi ipi kwa maana ya uzoefu, elimu na uwezo wao wa kufanya kazi.

“Mjadala huu unatokana na wasiwasi usio halali, kama ukidai kuwa wakurugenzi ni makada wa chama na kwamba wanakwenda kukisaidia chama, binafsi nakataa kwa sababu hawa wote wana taratibu zao za utendaji ambazo zipo wazi, hata kama ni uchaguzi mkuu taratibu za sheria ya uchaguzi mkuu zipo na zinasimamiwa na NEC),” alisema.

Pia alipongeza kwa kusema kuwa uteuzi wa wakurugenzi pamoja na makatibu tawala ni sawa na promosheni kwa mtumishi wa umma.

Kwa upande wake, Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwa kifupi kwamba siku zote uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri pamoja na makatibu tawala umekuwa ukiwalenga makada wa chama tawala.

“Si jambo geni kwa rais kuteua makada wa chama tawala kushika nafasi hizo, Mzee Mkapa alifanya hivyo, Kikwete naye alifanya hivyo, labda kitu kigeni hapa ni kwamba Magufuli ameteua kwa uwazi kuliko watangulizi wake ambao waliteua kimya kimya,” alisema Profesa Mkumbo.

Naye Mbobezi wa Sayansi ya Siasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema uteuzi huo wa Magufuli unaakisi hoja ya kwamba watumishi wa umma wamegeuzwa kuwa watumishi wa chama tawala.

Profesa Baregu alisema hali hiyo inatokana na Magufuli kuwa na mamlaka makubwa ya uteuzi, hivyo jamii haijui wateuliwa hao wanakwenda kushika nafasi hizo kwa lengo gani.

Alisema madhara ya Magufuli kupewa mamlaka makubwa ya uteuzi ni kuteua watu bila kufuata weledi bali kuangalia matakwa ya chama chake.

“Watu hawa wanateuliwa kwa matakwa ya chama tawala, uteuzi umefanyika pasipo kuangalia halmashauri inahitaji mtu wa aina gani hivyo matokeo yake hakutakuwa na maendeleo bali wateule hawa wataheshimu chama badala ya dola,” alisema Profesa Baregu.

Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, kwa njia ya simu ya mkononi ili kutoa ufafanuzi wa vigezo vilivyotumika kuwateua Ma-DED hao lakini hawakupokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles