SHIRIKA la kimataifa linalowashughulikia watoto “Save the Children” limesema kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa katika maeneo yenye migogoro kila mwaka inazidi kuongezeka, hali ambayo inaathiri makuzi na maendeleo yao.
Shirika hilo limebainisha kuwa kila mtoto mmoja kati ya watano wanakulia katika maeneo ya mizozo, ikiwa ni kiwango cha juu kuliko miaka ya nyuma.
Mnamo mwaka 2017 watoto milioni 420 walisumbuliwa na vita na mizozo kote ulimwenguni. Shirika la Save the Children linawataja watoto wanaoishi Afghanistan, Yemen, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa ndio wanaoishi katika hali ya hatari zaidi.
Shirika hilo limetoa wito uchunguzi huru ufanyike ili kutambua kama haki za binadamu na hasa za watoto hazijakiukwa. Ripoti ya Save the Children imetolewa mjini Munich, kunakofanyika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama.