25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto wanaobalehe kupima Ukimwi

hiv-test_header

Na NORA DAMIAN-DAR ESSALAAM

WATOTO wanaobalehe huenda wakaruhusiwa kupima virusi vya Ukimwi (VVU) ili kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyomo katika mwongozo wa uwekezaji kwenye Ukimwi ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS).

Shirika hilo limeweka malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 na nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, tayari zimeanza utekelezaji kuhakikisha zinafikia malengo hayo.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu juzi, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa tume hiyo, Richard Ngilwa, alisema hivi sasa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 haruhusiwi kupima bila idhini ya wazazi au walezi wake.

Kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ukimwi ya mwaka 2008, mtoto ama mtu asiyeweza kupokea majibu ya vipimo vya VVU kama vile mlemavu wa akili, mzee asiyejitambua, mgonjwa asiyejiweza kiakili na wengine wenye shida kama hizo, anaweza kupimwa kwa ridhaa ya maandishi ya wazazi ama walezi.

“Mwongozo una mambo mengi na mojawapo ni hilo la kupima ambapo tumependekeza mtu anapopima na kukutwa na VVU aanze dawa mara moja, umri wa kuanza kupima ushushwe hadi miaka 15 na adolescence (waliobalehe) nao waruhusiwe kupima,” alisema Ngilwa.

Alisema utekelezwaji wa mwongozo huo utaanza baada ya kufanyika tathmini ya mkakati wa kudhibiti Ukimwi wa 2013/14 hadi 2017/18, ambayo itafanywa mwanzoni mwa mwaka ujao.

Ngilwa alisema yapo mafanikio kutokana na mkakati huo kama vile upatikanaji rahisi wa huduma za upimaji na unasihi, kutokomeza VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, upatikanaji wa kondomu za kiume na kike nchi nzima, tohara kwa wanaume katika mikoa 12 iliyoonekana kuwa na kiwango cha chini cha tohara.

Kuhusu utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi ambao unaendelea kufanyika, alisema wanatarajia matokeo yatatolewa baada ya miezi minane kuanzia sasa.

Utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania wa mwaka 2016/2017, unafanyika katika nchi 20 Afrika na kwa sasa nchi nane zinaendelea na utafiti huu zikiwamo Zimbabwe, Zambia, Malawi, Lesotho, Swaziland, Uganda, Namibia na Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles