BEATRICE MOSSES-MANYARA
WATAALAMU wa masuala ya afya mkoani Manyara wameombwa kupita vijijini na kutoa elimu dhidi ya na kuwakagua watoto wanaofikishwa kliniki kuona kama wamekeketwa.
Ombi hilo lilitolewa juzi kwenye mdahalo wa kusafisha mkoa dhidi ya ukeketaji na kupinga ukatili dhidi ya vitendo hivyo ulioandaliwa na Shirika la World Vision uliofanyika mjini Babati mkoani Manyara, mwishoni mwa wiki.
Mchungaji Stanley Minde alisema kama ukaguzi huo utawekwa na kutiliwa maanani tatizo la ukeketaji litapungua au kuisha kwa vile kwa sasa baadhi ya wazazi wamekuwa wakisingizia kwamba mtoto anapata ‘kilawalawa’ lakini pia wamiliki wa madini wanaamini kiungo hicho kikiwekwa mgodini, watapata mafanikio makubwa.
“Suala la ‘kilawalawa’ limekuwa kisingizio kikubwa, wanaposema mtoto anazaliwa na kilawalawa baada ya muda wanajifanya wanakwenda kukitoa.
“Lakini hata kama watatoa hicho kilawalawa ni lazima akaguliwe na hii inatakiwa kuwa propramu maalumu hospitalini, hakika ukatili huo hautakuwapo tena,” alisema Minde.
Meneja wa World Vision Babati, Majid Mfinanga alisema kulingana na takwimu za mwaka 2015, asilimia 10 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 wamekeketwa nchini.
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa ukeketaji katika taifa kuwa ni Manyara asilimia 58 wakati wilaya inayoongoza kwa ukeketaji watoto wa kike ni Babati.
“Sote tunatambua kuwa vitendo vya ukeketaji vinachangia kwa kiasi kikuwa kuhamasisha ndoa na mimba za utotoni.
“Lakini tunahakikisha kwamba chochote tunachokifanya katika jamii mwisho wa siku ni lazima kimguse mtoto kumlinda dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kumletea madhara ya mwili au saikolojia maishani mwake,” alisisitiza Mfinanga.