Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Zaidi ya watoto milioni 8.5 wenye umri wa miezi sita mpaka miaka mitano wanatarajiwa kupatiwa matone ya Vitamin A na dawa za kutibu maambukizi ya minyoo ili kulinda afya na maendeleo yao.
Utoaji wa huduma hizo ni utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ijulikanayo kama ‘Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto’ ambayo hufanyika kila baada ya miezi sita yaani Juni na Desemba kila mwaka.
Akizungumza juzi Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Elifatio Towo, amesema Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto ni mojawapo ya mikakati ya kulinda afya na maendeleo ya mtoto.
Amesema katika kipindi hicho huduma jumuishi za afya na lishe hutolewa kwa mtoto mwenye umri kuanzia miezi sita hadi miaka mitano ambazo ni pamoja na matone ya Vitamin A, dawa za kutibu maambukizi ya minyoo, upimaji wa hali ya lishe, utoaji ushauri nasaha na kutoa rufaa kwa mtoto anayebainika kuwa na utapiamlo mkali.
“Licha ya jitihada nzuri zinazochukuliwa na serikali katika kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa huduma zinazotolewa katika Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto bado kuna watoto ambao hawajafikiwa na huduma hizi, hivyo kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha wananchi ili waweze kuwapeleka watoto wao wenye umri wa kuanzia miezi sita mpaka miaka mitano kwenye vituo vya kutolea huduma,” amesema Dk. Towo.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa huduma za Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto, Francis Modaha, amesema wanatarajia kuwafikia walengwa kwa zaidi ya asilimia 90.
“Watoto wana maradhi mengi hivyo tunapotoa huduma hizi kwanza tunaokoa muda wa wazazi na watoa huduma kwa sababu watoto wanaletwa pamoja na kupata huduma kwa pamoja, tutapunguza vifo vya watoto na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa huduma zitolewazo wakati wa Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto,” amesema Modaha.
Akitoa mada kuhusu umuhimu wa Vitamin A mwilini Mtaalamu kutoka katika taasisi hiyo, Wessy Meghji, amesema upungufu wa madini hayo husababisha mtoto kuugua mara kwa mara na kutopona haraka, ukuaji hafifu na maendeleo ya mtoto, vifo, kutoona vizuri katika mwanga hafifu, mtoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa, kuharisha na magonjwa ya mfumo wa hewa.
Amesema ili kukabiliana na upungufu wa Vitamin A wamekuwa wakihamasisha unyonyeshaji maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na kuendelea hadi miaka miwili na zaidi, kumpa mtoto aliyefikia umri wa miezi sita vyakula vya nyongeza, matone ya Vitamin A na kutoa elimu ya lishe kuhusu umuhimu wa madini hayo na yanakopatikana kwa wingi.
“Vyakula tulavyo havikidhi mahitaji ya Vitamin A kwa watoto kwani hula kiasi wakati mahitaji yao ni makubwa hivyo, ni muhimu wapatiwe Vitamin A ya nyongeza mara mbili mwaka,” amesema Meghji.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano wa TFNC, Freddy Lwoga, amesema taasisi imekuwa ikiendesha semina kwa wanahabari kwa lengo la kuwajengea uwezo waweze kuelewa masuala ya lishe kwa sababu wengi wanapenda kuandika habari hizo.
“Tulibaini kuna kundi kubwa halijafundishwa kupitia press club (Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam), ndiyo maana tumeamua kutoa mafunzo haya ili wapate maarifa ya kutosha na kuandika habari halisi hasa kuhusu huduma zitolewazo katika Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto,” amesema Lwoga.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC), Irene Mark, ameishukuri TFNC kwa kutoa mafunzo hayo na kuahidi kuwa wanachama wa klabu hiyo watakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya lishe ya mtoto.